Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tishio la ndumba uwanjani liko hivi...

Simba Ushirikina.jpeg Tishio la ndumba uwanjani liko hivi...

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Historia ya mambo ya ndumba au juju ama kwa neno sahihi zaidi ni imani za kishirikina ambazo katika soka la Bongo haikuanza leo wala jana, bali ni tangu miaka hiyo ya uanzishwaji wa Ligi Kuu Bara.

Mtakumbuka miaka ya 1990-2000 Simba na Yanga zilitikisa katika soka la Afrika, na jarida moja la michezo barani Afrika liliandika kuhusiana na juju likimaanisha imani za kishirikina katika soka la Tanzania.

Kwa utafiti wa kuona kwa macho tu, ndumba au juju katika soka la Bongo huwa na lengo la kusaka ushindi na sio kumdhuru mchezaji wa timu pinzani.

Hata katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Jumamosi kati ya Simba na Raja Casablanca tukio la basi la Simba kudaiwa kuingia kwa mtindo wa kinyume nyume lilizua maswali na mitandaoni likahusishwa na imani kama hizi. Hata hivyo, taarifa hizo zilikanushwa.

Swali la msingi ambalo linabaki katika akili zetu ni je imani hizo za ndumba zinaleta mafanikio katika soka? Jibu ni rahisi na kila mdau wa soka analo.

Kama ni kweli ndumba au juju zinaleta ushindi, basi Tanzania na klabu za soka zinazoshiriki mashindano makubwa kama ya CAF zingekuwa zimefanya makubwa katika soka duniani.

Haijawahi kuthibitika iwapo ndumba ni nyenzo muhimu ya ushindi kwa klabu za soka hapa nchini, na kama kweli inasaidia ushindi, basi mchango wake sio wa moja kwa moja zaidi ya kwamba ni kuibua athari za kisaikolojia kwa timu pinzani.

Kutengeneza tishio la ndumba ambalo linazaa hofu kwa mpinzani wako ni mojawapo wa mbinu za kumshinda kirahisi.

Historia ya tamaduni, mila na desturi za baadhi ya maeneo hapa nchini kama vile ya Ukanda wa Pwani mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pemba na Unguja yanaonyesha uwepo wa imani kubwa ya ndumba katika soka.

Maeneo hayo kuanzia zile ligi ndogo za mchangani ni kawaida kukuta matukio ya hapa na pale ya kuvunjwa vitu uwanjani au kukwepa eneo kuu la kuingilia uwanjani ama kubeba vitu kama hirizi na kadhalika.

Lakini ipo pia tabia au desturi ya mashabiki kindakindaki au wakereketwa ama vikundi vya uhamasishaji kuvaa na kuwa na vitu ambavyo huashiria kama vile ni vya kishirikina, lakini inakuwa sio kweli bali lengo lao ni kuwapa hofu wapinzani.

Katika kitabu kilichoandikwa na mwanaanthropolojia wa Ujerumani 2011 ajulikanaye kama Lisa Mackenrodt ambaye alitafiti mambo mbalimbali na wataalamu wa mambo ya uganga wa kienyeji wa maeneo ya Pwani, alithibitisha hayo.

Kitabu hicho kinachoitwa “The Jinn Fly on Friday” kinaeleza mambo ambayo aliyapata kutoka kwa watalaamu hao wa Ukanda wa Pwani ambao wapo wa aina tatu wakiwamo wanaotumia vitabu, tunguli na mitishimba.

Ingawa pia wapo ambao ni wanaotumia mchanganyiko wa aina mbalimbali za uganga.

Mwandishi Lisa anaeleza kuwa kuna imani kubwa iliyojengeka kwa watalaamu hao wa vitabu na tunguli katika kusaidia matatizo mbalimbali yanayowakabili kwenye maisha ya kila siku kwa jamii za Kiswahili za Pwani ikiwamo magonjwa, mapenzi na biashara.

Hivyo haishangazi kwa yale ambayo yanaonekana katika soka la Tanzania pale unapoona viashiria visivyo vya kawaida vinaonyesha kuwa kuna imani kubwa katika ndumba.

Viashiria vya imani katika ndumba ni vingi ikiwamo kukwepa kuingia milango mikubwa na kuruka ukuta, kuingia kinyume nyume uwanjani, kuchoma moto, kupasua mayai au nazi viwanjani.

Vilevile wapo wachezaji ambao wamewahi kuonwa wakiwa wamebeba vitu katika miili yao au kufungwa. Vitu hivyo hujulikana kama hirizi na vinahusishwa na mambo ya ndumba.

Tishio la ndumba huleta hali fulani ya ajabu.

Kutokana na kuenea kwa taarifa potofu mbalimbali zinazohusu ndumba au juju katika jamii ni kawaida huleta hofu au taharuki pale wanapoona au kusikia kuwa leo timu fulani imetoka kufanya mambo hayo.

Kwa upande wa jicho la tatu la kitabibu ni kuwa ndumba au juju ama mambo yanayoashiria ushirikiana yanaweza kuleta tishio kwa binadamu na hatimaye kumsababishia matatizo ya kisaikolojia. Mchezaji pale anapokuwa na hofu kutokana na tishio la ndumba ni kawaida kushindwa kucheza kwa kiwango cha juu kwani unapokuwa na hali ya hofu au woga umakini unakosekana uwanjani.

Tishio la uwepo wa ndumba au mambo ya kishirikina huwapa hofu wachezaji ambao wamewahi kusikia kuwa vitu hivyo vinaweza kuwa na madhara au kuwasababishia hata vifo.

Kuingiwa na hofu au woga pekee tayari ni zaidi ya ndumba au juju kwani mchezaji mwenye hali hiyo anaweza kucheza pasipo kujiamini, kutokuwa makini na kukosa ari au hamasa.

Tishio la ndumba kwa wachezaji huweza kuzaa hofu iliyopitiliza ambayo huambatana na wasiwasi au woga juu ya maisha ya kila siku katika soka bila hata sababu ya msingi.

Mara nyingi hofu inapokuwepo kwa binadamu humfanya ahisi kuwa kuna janga kubwa litampata. Kwa mchezaji hii inaweza kumfanya ashindwe kuwa sawa uwanjani.

HOFU YA NDUMBA INAKABILIWAJE?

Kwa mwanasoka mwenye hofu ya kuathiriwa na ndumba au imani za kishirikina anahitaji kusaidiwa na wanasaikolojia wa timu kwa ajili ya kumpa ushauri tiba.

Ushauri huo hufanyika ili kumjengea imani na kumwondolea hofu ya ndumba. Mchezaji anatakiwa kushikamana na imani ya kidini kwani inasaidia kutoogopa matukio ya ndumba uwanjani.

Jambo jingine ni mshikamano wa viongozi wa timu na wachezaji ili kurudisha ari na hamasa katika kikosi chao. Hapa viongozi wenye ushawishi wanahitajika kuzungumza na wachezaji ili kuwatoa hofu inayotokana na imani za ndumba.

CHUKUA HII

Ndumba sio nyenzo ya moja kwa moja ya kupata ushindi uwanjani, bali huleta athari tu za kisaikolojia ikiwamo kuwapa hofu wapinzani. Muhimu ni kutojenga imani kuwa ndumba ndio nyenzo kuu ya ushindi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live