Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu zitakazopanda Ligi Kuu presha juu

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku saba kabla ya kuanza mechi za mchujo kusaka timu mbili za ziada zitakazocheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao na mbili zitakazoshuka daraja, presha imeanza kupanda.

Namungo FC iliyoongoza Kundi A, Polisi Tanzania Kundi B zimepanda Ligi Kuu na vita imehamia kwa timu nne za Ligi Daraja la Kwanza zilizoshika nafasi ya pili na tatu kwenye kila kundi.

Timu hizo nne zitagombea nafasi mbili za kupanda msimu ujao kwa kucheza na timu zilizoshika nafasi ya 17 na 18 katika Ligi Kuu.

Kutoka Kundi A timu zilizopta nafasi ya kucheza mechi za mchujo ni Mbeya Kwanza ya Mbeya na Mlale FC ya Ruvuma. Kundi B ni Pamba ya Mwanza na Geita Gold ya Geita.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana, baadhi ya makocha na viongozi wa timu za Ligi Daraja la Kwanza wameonekana kuanza kupata joto la mechi za mchujo ingawa walitamba kuwa wana imani ya kupata nafasi mbili za kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

“Tumeanza mikakati kwa sababu muda wenyewe hautoshi. Nimewaandaa wachezaji kisaikolojia kwa kuwaambia kuwa hiyo ni nafasi yao kuwa na majina makubwa na kuingia kwenye Ligi Kuu ambayo ni daraja la juu la soka. Tunaamini kila kitu kinawezekana kama hesabu zikienda vizuri tutatimiza lengo,” alisema Kocha wa Mlale Maka Malwisi.

Kocha wa Geita Gold, Hassani Banyai alisema ingawa timu yake ilistahili kupanda moja kwa moja, bado hawajakata tamaa na watahakikisha wanacheza Ligi Kuu msimu ujao.

“Kama mechi zilizomalizika zingefuatiliwa kwa ukaribu naamini tungepanda daraja lakini mwisho wa siku timu ambayo haikuwa na ubora ndio imepanda. “Kuhusu maandalizi ya kucheza mechi za mchujo yanaendelea vizuri na hatuna hofu tunachohitaji dhidi ya Mlale ni kushinda mechi zote mbili za nyumbani na ugenini, uwezo tunao kwasababu katika mechi za makundi tulizocheza ugenini, tulishinda michezo sita ikiwemo minne dhidi ya timu za majeshi,” alisema Banyai.

Mmiliki wa Mbeya Kwanza, Shiraz Bhachu alisema ingawa mfumo wa kucheza mechi za mchujo dhidi ya timu za Ligi Kuu unaziminya timu za Ligi Daraja la Kwanza, wapo tayari kupambana.

“Ligi yetu haina mdhamini tumetumia gharama kubwa kutukutanisha na timu za Ligi Kuu sidhani kama ni sahihi kwa sababu wenzetu ingawa hawana mdhamini mkuu, lakini angalau wanaonja fedha za udhamini hivyo timu inaweza kuona haina cha kupoteza kwenye ligi ikaamua kujipanga kucheza mechi za mchujo”, alisema.

Alisema pamoja na changamoto hizo wanaendelea na maandalizi na timu ipo kambini ingawa wana wachezaji majeruhi watano waliokosa mechi nne zilizopita.

Kwa mujibu wa ratiba, Mei 15 Mbeya Kwanza itacheza na Pamba FC kabla ya kurudiana Mei 22 mkoani Mwanza na mshindi wa mechi mbili baina yao atakutana na timu itakayoshika nafasi ya 18 kwenye Ligi Kuu katika mechi mbili zitakazochezwa Juni 2 na Juni 8. Mshindi atakata tiketi kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Tarehe hizo ndizo ambazo zitahusisha michezo miwili baina ya Geita Gold dhidi ya Mlale FC na mshindi baina yao atacheza dhidi ya timu itakayoshika nafasi ya 17 katika Ligi Kuu na mshindi atakata tiketi kucheza mashindano ya Ligi Kuu msimu ujao.



Chanzo: mwananchi.co.tz