Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu 60 kuwania ubingwa wa mbio za mitumbwi Kanda ya Ziwa

Mbio Za Mitumbwa Mwanza Timu 60 kuwania ubingwa wa mbio za mitumbwi Kanda ya Ziwa

Sun, 10 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Timu 60 za wanawake na wanaume kutoka wilaya 11 za mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera na Mara zitachuana kusaka mshindi wa mbio za mitumbwi Kanda ya Ziwa zitakazoanza Septemba 16, mwaka huu wilayani Misungwi na kuhitimishwa Desemba 9, 2023 katika Soko la Mwaloni Kirumba, wilaya ya Ilemela, Mwanza.

Mbio hizo zinalenga kutoa burudani kwa wananchi na kunufaisha washiriki kwa kujishindia zawadi mbalimbali zikiwamo nyavu za kuvulia, injini za boti na fedha taslimu, kukuza utalii na kutangaza utamaduni wa Kitanzania hasa katika Kanda ya Ziwa, kuhamasisha kujikinga na magonjwa hatarishi kama Malaria na Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa vijana ambao ni washiriki wakubwa katika mashindano hayo.

Akizungumza leo Septemba 9, 2023 katika bonaza la uzinduzi wa mbio hizo katika eneo la Kamanga jijini hapa, Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Mitumbwi Mwanza, Ludovick Mtesigwa amesema mashindano haya yataanza Septemba 16, mwaka huu wilayani Misungwi ambapo wilaya 11 zikiwamo nane za mkoa wa Mwanza na tatu za Geita, Musoma na Bukoba kila moja itatoa washindi watano watakaoshiriki fainali jijini Mwanza.

“Tunawaasa washiriki wengi wajitokeze kujiandikisha katika vituo vyote vya usajili vya kanda ya ziwa kwa ajili ya mashindano haya, usajili umefunguliwa rasmi katika kila wilaya na washiriki wanatakiwa kufika maeneo husika ili kukamilisha usajili wao, mwisho wa usajili wa washindani itakuwa siku tatu kabla ya shindano la wilaya husika kufanyika,” amesema Mtesigwa

Mshiriki wa mbio hizo, Grace Charles kutoka Ilemela amesema “ni mwaka wa nne nashiriki mashindano haya mwanzo niliyachukulia kama burudani lakini sasa imekuwa fursa na chanzo cha kipato changu, tunawaomba wadhamini waongeze nguvu watuangalie kwenye malipo na posho watupe kwa wakati,”

Meneja Matukio na Udhamini TMC wanaoratibu mbio hizo, Ibrahim Kaude, amesema wanaendelea kutafuta wadau ili kuyafanya mashindano hayo yapige hatua na kufika mbali ili timu ziweze kujiendesha kama ilivyo kwenye soka na kupata timu ya taifa itakayoweza kushiriki mashindano ya kimataifa ya mitumbwi.

“Matumaini yetu ni kuona mchezo huu unakwenda kuwa mchezo maarufu na wenye wapenzi wengi nchini, tumejipanga kuandaa mashindano bora kabisa yenye kuzingatia hadhi na taratibu za mchezo huu, tunatoa wito kwa wadau na wakazi wote wa Kanda ya Ziwa kujitokeza kwa wingi katika fainali za mashindano haya Desemba 9, 2023 Soko la Mwaloni, Mwanza,” amesema Kaude

Naye, Mwakilishi wa Jembe Development, Raymond Cuthbert amesema “mashindano haya yanawaongezea kipato washiriki na kutengeneza mahusiano ya kazi nasi tumeshiriki ili kuutangaza mchezo huu ufikie lengo lililokusudiwa, tumejipanga vizuri mambo yote yaliyoahidiwa zikiwemo zawadi zitatolewa kwa wakati na tunatamani watu wajitokeze kwa wingi tuutangaze mchezo huu ukue na kutoa ajira kwa watu wengi,”

Chanzo: Mwanaspoti