Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu 10 zakalia kuti kavu ligi kuu

51471 Pic+ligi+kuu

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Yanga, Azam na Simba zikichuana kileleni kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu 10 zipo katika hatari ya kuteremka daraja msimu huu.

Yanga inaongoza kwa pointi 71, Azam (63) na Simba (57) na moja kati ya hizo inapewa nafasi ya kutwaa ubingwa unaotoa fursa kwa timu kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimamo wa ligi hiyo unaonyesha timu hizo 10 zimepishana kwa idadi ya pointi moja au mbili hatua inayoonyesha kutakuwa na mchuano mkali katika mechi zao zijazo.

Kwa mantiki hiyo timu hizo hazina namna zinapaswa kucheza karata zao vyema katika mechi zao zijazo ili kujinasua na janga la kucheza Daraja la Kwanza msimu ujao.

Kutokana na ukaribu wa pointi baina ya timu moja hadi nyingine, ni wazi ushindani wa mechi zinazofuata kwa timu hizo zitakuwa na ushindani mkali kwa kuwa kila moja itahitaji pointi tatu muhimu.

Timu zenye hatari ya kushuka daraja ni JKT Tanzania yenye pointi 39, Singida United (39), Stand United (39), Mwadui (37), Alliance (37), Mbao (37), Kagera Sugar (36), Ruvu Shooting (36), Biashara United (34) na African Lyon (22).

Timu mbili tu kutoka mwisho kwenye msimamo wa ligi ndizo zitashuka daraja lakini nyingine mbili zinazofuata zitacheza mechi za mtoano na timu mbili zitakazoshika nafasi ya pili kwenye makundi mawili ya Ligi Daraja la Kwanza na ambazo zitafungwa zitaungana na mbili kushuka daraja.

African Lyon kama itapoteza mchezo mmoja tu katika mechi zake tano zilizobaki itashuka daraja moja kwa moja kwa kuwa hata kama ikishinda mechi zitakazofuata itafikisha pointi 34 ambazo ni pointi za Biashara United kwa sasa. Pia Biashara United ambayo iko nafasi ya pili kutoka mkiani kwa pointi 34 kama itashinda mechi zote saba itafikisha pointi 55.

Ingawa timu hiyo imebakiza michezo saba lakini ina kibarua kigumu cha kuvikabili vigogo Simba na Yanga itakapokutana nazo. Timu hiyo ina mechi mbili dhidi ya Simba ya mzunguko wa kwanza ambayo ilipaswa kufanyika jana kabla ya kuvaana tena Aprili 25. Pia ina mechi dhidi ya Yanga iliyopangwa kufanyika Mei 5 kabla ya kuzivaa Ruvu Shooting, Alliance, Lipuli na Mbeya City ambazo zinapambana kubaki Ligi Kuu. Kagera Sugar inayonolewa na kocha bora msimu wa 2016/2017 Mecky Maxime haiko salam, inashika nafasi ya 17 ikiwa na pointi 36. Endapo itashinda mechi saba zilizobaki itafikisha pointi 57.

Hata hivyo timu inakabiliwa na mfupa mgumu wa kupambana na Simba na Yanga ambazo zinazochuana kuwania ubingwa.

Kagera itaanza na Yanga Aprili 11 na Aprili 19 dhidi ya Simba kabla ya kumenyana tena na Simba Mei 9.

Kauli za makocha

Kocha wa African Lyon Salvatory Edward alisema wako katika nafasi mbaya, lakini wataendelea kupambana hadi dakika ya mwisho kwa kuwa mchezo wa soka hauna mwenyewe.

“Licha ya kwamba tuko mkiani kwenye msimamo wa ligi haitukatishi tamaa bali inatupa moyo wa kupambana,”alisema nahodha huyo wa zamani wa Yanga.

Kocha wa Alliance Malale Hamsini alidai timu yake haitashuka daraja kwa kuwa ahadi yake haijatimia licha ya kukiri ligi ni ngumu na wako katika nafasi mbaya.

Kocha wa Prisons, Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema licha ya kwamba timu yake iko nafasi ya sita ikiwa na pointi 42 lakini bado hawako salama. “Bado ligi ngumu hata sisi hatuko salama licha ya kwamba tuko nafasi ya sita kwasababu kuanzia wa pili kutoka chini wana nafasi ya kufikia pointi zetu,”alisema Rishard.



Chanzo: mwananchi.co.tz