Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tenga: Motisha ndio itaibeba Serengeti Boys

32889 Pic+serengeti Tanzania Web Photo

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tanzania imepangwa Kundi A na timu za Nigeria, Angola na Uganda katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa vijana chini ya miaka 17 huku kundi B likiwa na timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Mashindano hayo ya Afcon kwa vijana yatafanyika Aprili 14 hadi 28 mwakani jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Serengeti Boys itafungua dimba dhidi ya Nigeria wakati Uganda itacheza na Angola. Kundi B Guinea itaanza na Cameroon wakatiSenegal itacheza na Morocco.

Akizungumza baada ya droo hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Leodegar Tenga alisema kila timu ambayo imeingia katika mashindano hayo ilifanya vizuri kwahiyo hakuna timu ya kuibeza zaidi ya kufanya maandalizi ya kutosha. “Serengeti Boys ni timu nzuri ambayo inaweza kufanya vizuri, lakini wanatakiwa kupewa motisha ya kutosha ili waweze kupata maandalizi ambayo ndio yatakuwa silaha kubwa kwao kufanya vizuri katika mashindano ambayo yanafanyika hapa nyumbani kwa mara ya kwanza na kuweka historia,” alisema Tenga.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema walishaanza kuiandaa timu siku nyingi na katika kipindi hiki wapo katika muendelezo ili timu yao ifanye vizuri katika mashindano hayo.

“Timu itakuwa inacheza nyumbani na kwetu tumedhamiria kujiandaa ili kuleta ushindani na si kuwa washiriki, lakini tunaomba motisha na nguvu kutoka kwa wadau mbalimbali ili kupata maandalizi ya kutosha ambayo yatakuwa ni miongoni ya silaha muhimu kwetu,” alisema Milambo.

Kocha msaidizi wa Serengeti Boys Maalim Salehe alisema kama timu hiyo inaondoka kwenda kushiriki mashindano mengine bila kupata nguvu ya kutosha inachukua vikombe je kama watapata nguvu na motisha ya kutosha ndio itawapa nguvu ya kufanya vizuri zaidi.

“Tuna wachezaji wazuri ambao wapo pamoja muda mrefu na kama wakipewa motisha ikiwemo kuishi katika mazingara mazuri kupata vyakula vizuri na mambo mengine yote ya msingi tuna nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano ya Afcon mwakani,” alisema.

“Kundi hili kwetu ni rafiki na tuna nafasi kubwa ya kwenda nusu fainali ambapo tutakuwa tumeshapata nafasi ya kwenda kucheza Kombe la Dunia kwani tunawafahamu Uganda na Angola tumeshacheza nao ila Nigeria ndio wageni kwetu,” alisema Selehe.

Naye nahodha wa Serengeti Boys Morice Michael alisema “Kama wachezaji tumeliona kundi na kazi kubwa kwetu ni kuhakikisha tunapambana na kufikia yale malengo ya timu ya kufanya vizuri katika mashindano hayo ambayo yatafanyika hapa nyumbani,” alisema Michael.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema kufanya vyema kwa Serengeti Boys sababu kubwa wapo pamoja muda mrefu na hata katika mashindano mengi wamekuwa wakifanya vizuri hiyo ni dalili njema kwao.

“Kwangu naona wananafasi kubwa ya kufanya vizuri lakini si wao pekee yao ile ni timu ya Taifa kwa maana hiyo wanatakiwa kupewa nguvu na Taifa zima katika kila maeneo muhimu kwani uwezo wa kufanya vizuri wanao,” alisema Mkwasa.

Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Wallace Karia alisema kama uongozi ulishaanza mipango mikakati ya kuandaa timu hiyo katika mazingira sahihi siku nyingi na lengo kuu waweze kufanya vizuri ikiwezekana kuchukua ubingwa.

“Tumeiandaa timu zaidi na sasa watakwenda Uturuki kucheza mashindano ambayo yatakuwa yameandaliwa na FIFA yote hiyo ni kuhakikisha wanakuwa pamoja na kupata maandalizi ya kutosha, lakini kwetu uongozi tutawapa motisha pale itakapokuwa inahitajika,”

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe aliwashukuru CAF kwa kuwapa uenyeji wa mashindano hayo na aliwahakikishia kuwa yatafanyika salama na hawatawaangusha.

“Ili mashindano yawe mazuri ni lazima timu yetu ya Serengeti Boys ifanye vizuri na kufika hatua za mbele na kwa upande wa Serikali tunaahidi kuwa nao bega kwa bega na kuwapa nguvu muda wote hadi mashindano yatakapomalizika,” alisema Dk Mwakyembe.



Chanzo: mwananchi.co.tz