Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tattoo za Wawa Simba zina maana kubwa

78964 Wawa+pic

Tue, 8 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

HUWEZI kuamini lakini huu ndio ukweli wa mambo kuwa, beki wa kati Muivory Coast Pascal Wawa mwili wake una tattoo zaidi ya 20 huku mwenyewe akifichua kwamba, kuna wakati husahau hata idadi kamili.

Wawa, ambaye tangu ajiunge na Simba huu ni msimu wa pili lakini kabla aliichezea Azam FC msimu wa 2013-2014 na baada ya hapo alitimkia zake klabu ya El Merreihk ya Sudan.

Kwa asiyemjua, ukikutana naye kwa mara ya kwanza unaweza kushangaa na ukajiuliza, huu ni mwili au daftari la kuandikia mtoto wa darasa la pili kwa jinsi ulivyojaa michoro ya tattoo kila kona.

Ana tattoo zinazoonekana katika kila sehemu ya mwili wake ndogo na kubwa kama miguuni, mapajani, kifuani, tumboni na hata shingoni.

Jambo linalofanya mwili wake ambao umeimarika kwa mazoezi na staili yake ya nywele ambayo hunyoa pembeni na kubakisha katikati afanane na watu wa mbele yaani wachezaji na wasanii wakubwa.

Mwenyewe anasema, bado anaendelea kuchora michoro mingine kama ilivyo kwa staa wa Barcelona, Artudo Vidal

Pia Soma

Advertisement
“Mwili wangu una tattoo nyingi zinaweza kuwa zaidi ya 20, kwa sababu tangu nimeanza kuzichora sijui hata idadi yake,” alisema Wawa ambaye ni baba wa watoto watano.

Alisema, tattoo alizochora alianza rasmi 2007 ni ya Dolphin. Ipo kwenye bega la mkono wa kushoto na kipindi hicho alipenda namna alivyokuwa anamwona mwanamuziki wa R&B, Cris Brown ama Nelly.

“Hii ndio tattoo yangu ya kwanza kabisa (anaonyesha) ndio nyingine zikafata. Na kuanza nilijikuta tu napenda,” anaeleza Wawa huku akifafanua sababu ya kumchora Dolphin ni kutokana na umuhimu wake majini, huwa ana tabia ya kusaidia watu pindi wanapokuwa wanataka kuzama.

Mbali na hiyo, Wawa amechora tattoo za familia yake yaani, watoto wake hao watano ambao ni Samira (12) Messie (10), Eliakim (7), Ryan (4) na Noah (1.3) pamoja na mkewe.

“Majina ya watoto wangu yote yako kwenye mwili wangu pamoja na mke wangu. Na hawa wadogo nimewachora kabisa sura zao kwenye mwili wangu,” anafafanua Wawa.

Alisema, amechora picha ya sura ya mkewe nyuma ya paja la mguu wa kushoto, nyingine kwenye kigimbi cha mguu wa kulia.

“Nampenda mke wangu ndio maana nimefanya hivyo, maana amekuwa mhimili mkubwa katika mafanikio yangu, anapokasirika mimi sifanikiwi kabisa kwenye kazi zangu,” anasema Wawa.

Kwenye paja la mguu wa kulia pembeni kuna sura ya mtoto wake mdogo Noah.

Pia, kwenye paja hilo la mguu wa kulia mbele kuna picha ya Mama Bikira Maria na paja la kushoto mbele Yesu.

Anasema, amefanya hivyo kutokana na imani yake ya Kikristo na mapenzi aliyonayo kwao.

“Tunaishi kwa imani, maisha yangu yanamtegemea Mungu kwa kila kitu na watu wanaweza kunichukulia poa, mhuni na nini, lakini siko hivyo,” anasema Wawa anayeweka wazi muda mwingi anaotumia kama hayuko na kambini huwa na familia yake.

Pia, amemchora jina la baba yake mzazi pamoja na mama yake.

“Sasa hivi nina mpango wa kuchora tattoo nyingine mkononi (anaonyesha) hii nimeipenda tu,” anasema Wawa na kusisitiza anataka mwili wake uwe kama mchezaji wa Barcelona Altudo Vidal.

Hata hivyo, pamoja na mastaa kupenda kuchora tattoo hizo nyingi, wapo wengine hawafanyi kabisa.

Mfano ni mshambuliaji wa Ureno na Inter Milan, Cristiano Ronaldo hachori kabisa.

Ronaldo aliweka wazi sababu ni kitendo chake cha kuchangia damu, inaelezwa unapochora tattoo hutaweza tena kuchangia damu kwa mtu mwingine.

HUMWAMBII KITU KUHUSU MKEWE

Wawa, ambaye anaishi maeneo ya Africana nje kidogo ya Dar es Salaam pamoja na familia yake yaani mkewe na watoto wake wawili wadogo ingawa kuna wakati wanaondoka kwao Ivory Coast na kumwacha akiendelea na majukumu ya kazi.

Alisema hapendi kumwona hana furaha kwa sababu anafanya kazi kwa ajili yake na amekuwa akihakikisha anapata huduma zote.

Hii ilijidhihirisha wiki mwishoni mwa wiki iliyopita, alikwenda kwenye duka moja maarufu la Falim Ayez

ambalo huuza pafyum, miwani na saa orijino na kununua saa mbili zenye kufanana tofauti ni ukubwa zenye gharama ya USD 500 zaidi ya Sh 1 milioni

moja ilikuwa ya mkewe na nyingine kubwa ilikuwa ya kwake na baada ya kununua aliivaa hapo hapo.

“Ninachopata tunatumia haya maisha tu huwezi kujua ya mbele, lakini pamoja na mimi kufanya yote haya, napenda kusaidia sana watu hata nyumbani kwetu Ivory Coast wanajua vizuri sana hilo.

Wakati anakwenda katika duka hilo, walitokea mashabiki wa Simba wakaomba kupiga naye picha wakapiga, wakati anarudi mahali alipokuwa amepaki gari yake wakati analipa aliambiwa nenda tu.

Hii ni baada ya shabiki wake kujitolea, jambo ambalo lilimgusa Wawa na kusema : “Unaona, huu ni upendo wa kweli, mtu huyu amelipa kiasi kidogo cha pesa Sh 500 tu lakini kwangu ina maana kubwa, hana kikubwa lakini ametoa kwa sababu ya mapenzi.”

AWATAJA MASHABIKI BONGO

anasema, amecheza soka nchi tofauti kama Sudan, Ivory Coast na hapa Tanzania lakini hawa wa Bongo ni balaa. Wanapenda soka.

“Sudan, Ivory Coast kuna wapenzi wa soka na wanapokuona ni vita lakini hapa Tanzania ni zaidi,” alisema Wawa.

USHINDANI WA NAMBA

“Jukumu langu ni kufanya kazi hivyo nataka watu wanijaji kwa kazi yangu uwanjani na si kwa maneno,” anasema Wawa.

Hata hivyo, katika kikosi chao wanaowania namba hiyo ni wengi ambao ni Mbrazil, Kennedy Juma, Erasto Nyoni na Yusuf Mlipili.

Amesema, kazi yao ni kuhakikisha Simba inabeba mataji mengi zaidi kwa sababu ndio jukumu lao.

DAKTARI AZUNGUMZA

Daktari Shita Samwel anasema, si mbaya kuchora tatoo lakini kwa anayetaka kuchora kuna mambo ambayo anatakiwa kuyajua

kabla ya kufanya maamuzi hayo.

“Kitu cha kwanza tattoo inachorwa kwa kutumia vifaa vyenye ncha kali hivyo, mtumiaji anatakiwa kuwa makini katika kuvitunza kwa sababu vinaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kama ukimwi na Homa ya Ini,” alisema Shita.

“Tatizo lingine linaweza kuwa aleji kwenye ngozi mtu kujikunja na mambo mengine kwani, uchoraji huo unaweza kufanya ngozi kucharuka baada ya kukutana na kitu kipya.”

Aliongeza yapo matatizo mengine kama la kujutia. Mtu anaweza kuchora tattoo halafu baada ya muda akawa haitaki tena, sasa anapoiona inaweza kumuumiza kisaikolojia au akaamua kuitoa ikamsababishia kovu kubwa kwenye mwili wake.

“Sijajua matirio ambayo yanatumika kuchora tattoo hizo ni aina gani kwani, wakati mwingine yapo yanayoweza kusababisha saratani. Lakini, katika hilo sina uhakika mpaka ufanyike uchunguzi wa matirio hayo,” anafafanua Dk. Shita.

WACHEZAJI WENGINE WALIOCHORA TATOO

PAPPY TSHISHIMBI

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Pappy Tshishimbi ni miongoni mwa waliochora tattoo tofauti katika mwili wake. Tshishimbi alikaririwa kuwa mwili wake una tattoo zaidi ya 10.

WILKER DA SILVA

Straika Mbrazil wa Simba, Wilker Da Silva. Ukitazama mwili wake umechafuka kutokana na kuchora sehemu kubwa ya tattoo.

Amechora tattoo tofauti.

KELVIN YONDANI (VIDIC)

Beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani ‘Vidic’ ni sehemu ya wachezaji ambao aliyeupendezesha mwili wake kwa tattoo. Yondani amechora tattoo hizo katika sehemu tofauti ukiwemo mkono.

ARTURO VIDAL

Kiungo wa Barcelona, Mchile Artudo Vidal ndiye mchezaji, ambaye Wawa anamkubali zaidi kwa wale wa nje ya nchi. Hii imesababisha hata mambo mengi ambayo wanayafanya yanafanana ndani na nje ya uwanja.

Mwili wa Artudo umechafuka kwa tattoo kuanzia shingoni, tumboni, mikononi na miguuni. Pia, staili zao za nywele kichwani pamoja na kufuga ndevu ni sawa. Artudo na Wawa wamenyoa nywele zote pembeni na wameacha chache katikati kama mstari.

Chanzo: mwananchi.co.tz