Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tariq aitumia salamu Simba SC, Yanga ikiichapa Biashara United

90391 Tariq+pic Tariq aitumia salamu Simba SC, Yanga ikiichapa Biashara United

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji Tariq Seif aliingia akitokea benchi na kuifungia Yanga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaiweka Yanga katika mazingira mazuri kabla ya mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya watani zao wa jadi Simba ambao leo watacheza dhidi ya Ndanda kwenye uwanja Taifa.

Mshambuliaji Tariq akicheza mechi yake ya kwanza aliingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya David Molinga alifunga bao hilo katika dakika 83 akiunganisha krosi iliyopigwa na nahodha Papy Tshishimbi na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Yanga.

Kwa dakika zake za kwanza, Tariq alionekana kukosa ujanja mbele ya James Mwasota na Abdulmajid Mangalo ambao walikuwa wakicheza mabeki wa kati wa Biashara United.

Ni kama alikuwa akiwategea Tariq kuwa wajisahau  ndicho kilichotokea mwishoni mwa kipindi hicho cha pili kwa kuifanya Yanga kujikusanyia pointi tatu wakiwa Uwanja wa Taifa.

Tariq ambaye alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi sita akitokea nchini Misri, mara baada ya kufunga bao hilo hakuonekana kushangilia na badala yake aliwataka Biashara wamsamehe kiishara kwa kunyoosha mikono juu.

Kabla ya kutimkia Misri ambako alikuwa akicheza soka la kulipwa mshambuliaji huyo, alikuwa akiichezea Biashara United ya mkoani Mara.

Pamoja na ushindi huo wa Yanga bado kocha Charles Mkwassa anakazi ya kufanya kwa siku chache zilizobaki kabla ya kuivaa Simba kutokana na washambuliaji wake kukosa umakini huku timu ikishindwa kucheza kwa mipango jambo lililowanyima raha mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ilikosa utulivu wa kutumia nafasi kadhaa walizopata dhidi ya Biashara United.

Washambuliaji David Molinga na Mrisho Ngassa walipata nafasi ya wazi, lakini ilishindwa kuzitumia wakiwa ndani ya 18 eneo la mlinda mlango wa Biashara.

 Molinga alipata nafasi mbili akiwa uso kwa uso na kipa Daniel Mgore kitendo cha kutaka kugeuka ili apige mpira ukaondoshwa na beki wa Biashara United.

Mpira umepooza si kwa Yanga wala Biashara United, hadi kwa mashabiki shamlashamla zao zilikuwa zimepooza tofauti na ilivyozoeleka hadi lilipopatikana bao.

Katika michezo mingine Coastal Union ikiwa nyumbani imeichapa Mbeya City kwa mabao 2-0 shukrani kwa magoli ya Shaaban Hamis na Ayoub Lyanga.

Uwanja wa Samora, Iringa wenyeji Lipuli imefanya kile kilichosubiriwa na mashabiki wake kwa kuichapa Mbao FC kwa mabao 3-0, wakati Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani imekubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Alliance FC huku Ruvu Shooting ikiitandika Kagera Sugar kwa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi.

Matokeo

Yanga Sc 1-0 Biashara United

Lipuli Fc 3-0 Mbao Fc

Coastal Union 2-0 Mbeya City

Mtibwa Sugar 0-1 Alliance Fc

Ruvu Shooting 2-1 Kagera Sugar

Chanzo: mwananchi.co.tz