Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tariq aanza kwa neema Yanga

90412 Tariq+pic Tariq aanza kwa neema Yanga

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Charles Mkwasa dhidi ya Biashara United, yamekuwa na manufaa kwa mchezaji mpya wa Yanga, Tariq Seif.

Tariq ameingia Yanga kwa mguu mzuri baada ya kufunga bao pekee katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, jana.

Mshambuliaji huyo jana alikuwa shujaa wa Yanga baada ya kufunga bao hilo dakika ya 83 ikiwa ni mechi yake ya kwanza kucheza tangu aliposajiliwa katika usajili wa dirisha dogo.

Tariq aliyeingia akitokea benchi kujaza nafasi ya David Molinga alicheza kwa ufanisi licha ya kukabiliwa na upinzani wa mabeki wa timu yake ya zamani ya Biashara.

Mchezaji huyo alisema bao hilo lina maana kubwa kwa Yanga kwa kuwa limeongeza pointi na kumuweka katika nafasi nzuri ndani ya kikosi hicho.

“Nilicheza nikiwa na lengo la kuisaidia timu yangu kupata ushindi, mchezo ulikuwa mgumu lakini tulipata nafasi moja tukaitumia,”alisema Tariq.

Mchezaji huyo alisema matarajio yake ni kufanya vyema katika mchezo ujao dhidi ya watani wao wa jadi Simba utakaochezwa Jumamosi wiki hii.

“Naiheshimu Simba kwasababu ni timu kubwa kama Yanga, lakini nikipata nafasi ya kucheza nitaongeza kiwango zaidi ya hapa,”aliongeza Tariq aliyekuwa akicheza soka Misri.

Katika mchezo wa jana, Yanga ilishindwa kutumia idadi kubwa ya nafasi ilizopata kufunga mabao kabla ya Tariq kuipa pointi tatu ambazo zimeifanya Yanga kufikisha pointi 24.

Kitendo cha Mkwasa kuwatoa Molinga, Feisal Salum, Mrisho Ngassa na kuingia Mapinduzi Balama, Papy Tshishimbi yalikuwa na manufaa kwa Yanga kwani kipindi cha pili iliongeza kasi ya mashambulizi.

Uhai wa Yanga uliboreshwa na Tshishimbi ambaye alicheza kwa uelewano na kiungo Abdulaziz Makame ambaye alikuwa akipenyeza mipira mirefu kwa mawinga wa pembeni.

Mawinga Deus Kaseke na Patrick Sibomana walitumia vyema pasi za Makame aliyeongeza kasi kutokana na muunganiko mzuri kati yake na Tshishimbi.

Pia Yanga ilibadili mbinu kwa kuwatumia mabeki wa pembeni Mustafa Suleiman na Adeyun Ahmed ambazo zilikaribisha mashambulizi langoni mwa Biashara.

Yanga: Meneta Mchata, Mustafa Selemani, Adeyun Ahmed, Lamine Moro, Ally Mtoni, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Feisal Salum, David Molinga, Mrisho Ngassa na Patrick Sibomana.

Biashara: Daniel Mgore, Wilfried Korouma, Novatus Dismas, DerrickMussa, Justine Bilary, James Mwasote, Abdulmajid Mangalo, Bright Obina, Mpapi Nassib, Ramadhan Chombo na Joseph Kimwaga.

Matokeo mengine katika mechi za jana, Lipuli iliichapa Mbao mabao 3-0, Coastal Union iliilaza Mbeya City 2-0, Ruvu Shooting iliinyuka Kagera Sugar 2-1 kabla ya Alliance kuigagadua Mtibwa Sugar bao 1-0.

Chanzo: mwananchi.co.tz