Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tarimba azipigia debe timu nchini

Video Archive
Thu, 16 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKURUGENZI wa Utawala na Udhibiti wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, ameyakumbusha makampuni ya michezo ya kubashiri matokeo kurudisha sehemu ya faida wanayopata kwa wananchi ikiwamo kudhamini timu za Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza.

Akizungumza kwenye ofisi za gazeti hili jana, ikiwa ni ziara yake kwa vyombo vya habari kushukuru kwa SportPesa kupokelewa vema na kuungwa mkono tangu kuanza shughuli zake miaka mitatu iliyopita hapa nchini, Tarimba aliweka wazi makampuni ya ubashiri yanapata faida kubwa.

"SportPesa tunathamini kile ambacho tunakipata, faida ambayo tunapewa na Watanzania tunairejesha kwao, njia moja wapo ni pamoja na kudhamini klabu za Ligi Kuu, tumekuwa wadhamini wa Simba, Yanga na Namungo," alisema Tarimba na kuendelea,

"Serikali inaweza ikaweka kipengele kwa makampuni yote kabla ya kupata leseni lazima wakubali kutoa sehemu ya faida yao kwa Watanzania kama ambavyo SportPesa tunafanya, timu zipo nyingi mpaka za Ligi Daraja la Kwanza," alisema Tarimba.

Aliongeza lengo la SportPesa si tu kuona kampuni inakuwa kibiashara, lakini kuona michezo hapa nchini inakua na ndio sababu wanafurahia mafanikio na timu wanazozidhamini.

"Timu zote tunazozidhamini zinafanya vizuri, hivi karibuni tutashuhudia mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (FA Cup), na timu zote zilizoingia hatua hiyo zinadhaminiwa na kampuni yetu (Simba na Namungo), haya yote kwetu ni mafanikio," Tarimba alisema.

Aliongeza anawashukuru Watanzania na wadau wa mpira pamoja na serikali kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya kampuni hiyo kwa muda wote tangu ilipoanza kutoa huduma zake hapa nchini.

"Tunawaahidi kuendelea kutoa huduma, lakini kuendelea kurejesha kwa jamii faida tunayoipata, kama nilivyosema lengo letu si tu kupata faida, lakini kuona michezo hapa nchini hususan mpira wa miguu unazidi kukua," alisema Tarimba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live