Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yapata pigo Olimpiki, wadau wavunja ukimya

15737 Pic+tanzania TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mvutano wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa la Kimataifa (AIBA), umeacha maumivu kwa mabondia wa Tanzania.

Mabondia wa Tanzania wataungana na wenzao duniani kote kutoshiriki michezo ya Olimpiki, baada ya kuibuka mzozo baina ya taasisi hizo kubwa. IOC imetoa msimamo wa kuondoa mchezo wa ngumi kwenye mashindano ya Olimpiki ijayo ya mwaka 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan baada ya mvutano wa zaidi ya miezi sita baina ya IOC na AIBA kabla ya kuchukua uamuzi huo juzi.

Kabla ya uamuzi huo, IOC ilizuia kamati za nchi mwanachama ikiwemo TOC kwa hapa nchini kutumia fedha za Kitengo cha Misaada (Olympic Solidarity) kwenye masuala ya ngumi kabla ya juzi kuamua kuondoa mchezo huo moja kwa moja kwa tuhuma za upangaji matokeo.

Uamuzi huo umeitikisa Tanzania ambayo tangu iliposhiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza mwaka 1964, timu za ngumi na riadha zilikuwa zikipewa nafasi kubwa ya kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki.

“Asili ya Olimpiki ni ngumi ukiondoa riadha, kitendo cha IOC kuiondoa michezo hii kimeshtua sijui ni kitu gani kimesababisha wasiafikiane, tulitarajia mvutano wao ungemalizika salama baada ya kupatiwa ufumbuzi.

“IOC ilipokuwa kwenye mazungumzo na AIBA ilituzuia kutumia fedha za ‘solidarity’ kwenye ngumi. Kushindwa kufikia mwafaka ni pigo hata kwetu Tanzania kuna vitu vingi tutakosa ,” alisema Makamu wa Rais wa TOC Henry Tandau.

Miongoni mwa athari ambazo Tanzania itazipata kwa uamuzi wa IOC ni timu ya Taifa kutoshiriki kwenye kambi maalumu ya Olimpiki ambayo kabla ya uamuzi huo ilitarajiwa kwenda kujifua kwa muda mrefu nchini Cuba.

“Pia makocha, waamuzi na viongozi wa ngumi hawatashiriki semina zote za IOC ambazo tumekuwa tukizitoa nchini, achana na kushiriki kwenye michezo yote ya Olimpiki ya wakubwa na vijana kwa kifupi tutakosa vitu vingi,”alisema Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi.

Bondia wa timu ya Taifa, Haruna Swanga alisema uamuzi huo umewashitua kwa kuwa umefuta mipango waliyoweka walipokuwa kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola, mwaka huu. “Tulikuwa tunajifua ili kufikia viwango vya Olimpiki tuliweka maazimio hayo tangu tulipomaliza Michezo ya Madola, lakini ndiyo hivyo,” alisema Swanga.

Mbali na Swanga mabondia waliowahi kushiriki Olimpiki ni Habibu Kinyogoli, Emmanuel Mlundwa na Haji Matumla kwa nyakati tofauti kila mmoja alionyesha kushtushwa na uamuzi wa IOC.

“Itabidi mabondia wetu wakubaliane na hali iliyotokea ni pigo kwao lakini hawana namna wajipange kwenye michezo mingine kama Afrika na Madola,” alisema Kinyogoli.

Mlundwa alisema uamuzi wa IOC ni ‘kifo’ cha wengi ingawa nchi inapata athari kwa kukosa misaada iliyokuwa ikipata.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT), Makore Mashaga alisema kuondolewa kwa ngumi ni pigo kwa Tanzania kwa kuwa ni mchezo wenye historia na Olimpiki.

Mashaga amewashauri mabondia nchini kutulia na kujipanga upya akiamini AIBA na IOC zina nafasi ya kukutana kutafuta suluhu ya tatizo hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz