Mabondia Tanzania, Paulo Ezra, Yusuf Changarawe na Mussa Maregesi wameihakikishia medali Tanzania kwenye michezo ya Afrika (All African Games) msimu huu.
Mabondia hao wa timu ya Taifa, wametinga nusu fainali na kujihakikishia medali za shaba kila mmoja bila kujali matokeo yao ya nusu fainali iliyochezwa usiku wa jana kwenye michezo hiyo inayoendelea mjini Accra, Ghana.
Kwa mujibu wa kanuni za ngumi za ridhaa kote duniani, mabondia wanaotinga nusu fainali, wote ni washindi wa medali, wale watakaopigwa hatua hiyo wanatwaa shaba na watakaoshinda, wanacheza fainali kusaka bingwa na mshindi wa pili.
Wote walipata ulingoni jana usiku, Maregesi akizichapa kwenye uzani wa Cruiser dhidi ya Oussama Kanouni wa Algeria, wakati Charangawe alitarajiwa kuvaana na Peter Kabeji wa DR Congo kwenye uzito wa kilo 80. Ezra alicheza juzi usiku na kupigwa kwa pointi 5-2 na Andrew Chilata wa zambia, lakini akiwa tayari ana uhakika wa medali.
Wakizungumza na gazeti hili moja kwa moja kutoka Ghana, mabondia hao, licha ya kueleza changamoto ya hali ya hewa ya joto kali, wamesisistiza haitakuwa kikwazo kushindwa kupambana na kufuzu kucheza fainali.
“Nilitamani kuwa bingwa kwenye uzani wangu, ndiyo plani kwa kila mmoja wetu hapa, akiwamo Changalawe na Maregesi, tuna ari kubwa sana ya kufanya vizuri, Watanzania nyumbani watuombee na sisi hatutowaangusha,” alisema Ezra.
Maregesi alisema, hakuna kinachoshindikana kwani nia yake ni kufika fainali, anajua anakwenda kucheza pambano gumu, lakini maandalizi aliyoyafanya tangu akiwa nchini anaamini yatamwongoza kutimiza ndoto yake.
“Naamini nitafanikiwa, japo kwa hali ya hewa ya huku ni joto sana, ukipangiwa kucheza michezo ya mchana saa 8 ambayo kwa sasa imesogezwa mpaka saa 10 jioni joto huwa ni kali, lakini hicho hakitakiwa kikwazo kwangu kupambana,” alisema.
Kete nyingine ya medali ilikuwa kwa timu ya kriketi ya wanaume, lakini jana ilikwama kutinga nusu fainali kwa kufungwa na Namibia kwa 72-71.
Allen ambaye ni mkuu wa msafara wa Tanzania akitokea Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alisema fursa nyingine ya medali ipo kwenye riadha.
Timu nyingine za Tanzania za soka la wasichana, kuogelea, judo, baiskeli na kriketi wanawake tayari zimeaga mashindano hayo na kurejea nyumbani kwa kupishana tangu juzi.
Timu hizo ziliondoshwa mashindanoni katika hatua za awali na kwa mujibu wa Allen, kwenye baiskeli, wachezaji wawili hawakumaliza mbio na mmoja hakushiriki baada ya kuugua mara tu baada ya kufika Ghana.