Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni, imesema ipo tayari kwa michezo ya pili ya soka la ufukweni itakayofanyika nchini Tunisia baadae mwezi huu.
Kocha wa timu hiyo Boniface Pawasa amesema atawaandaa vijana wake vizuri ili kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na wataitumia kama fursa kwao kung’ara.
Naye Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki nchini (TOC), Henry Tandau amesema wanaamini kutakuwa na uwakilishi mzuri wa timu ya Tanzania kwenye michuano hiyo hiyo.
"Imeonekana timu yetu ya soka la ufukweni ipo nafasi ya nane kwenye viwango vya ubora Afrika,hivyo tukafuzu kushiriki michuano hiyo, licha ya kwamba tumepata taarifa kwa kuchelewa lakini tutashiriki na tunaamini tutafanya vizuri," amesema Tandau.
Mkuu wa msafara wa timu ya Tanzania itakayoenda Tunisia, Suleiman Ame amesema anaamini hakuna kitakachowakwamisha kuelekea michuano hiyo.