RUFANI ya Tanzania dhidi ya majirani zao Uganda kutumia wachezaji wenye umri mkubwa katika mashindano ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana wa umri chini ya miaka 17 imefeli, imeelezwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, alisema rufani yao iliyokuwa inalalamika Uganda kutumia wachezaji watano wenye umri mkubwa 'imegonga mwamba' na hivyo Uganda itasonga mbele katika mashindano hayo.
Kidao alisema wamepokea kwa huzuni majibu ya rufani hiyo kwa sababu wanaamini Uganda ilitumia wachezaji 'vijeba'.
"Ni kweli majibu yametoka na tumeshindwa, hivyo Uganda wameshinda, nadhani hivi karibuni tutaliweka wazi hili," alisema Kidao.
Kiongozi huyo amewataka wadau wa soka la wanawake kuendelea kuziamini timu zao zote na shirikisho litaendelea kujipanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano ambayo bado hawajatolewa.
Yosso wa Tanzania waliondolewa katika mashindano hayo baada ya kuchapwa mabao 5-0 katika mchezo wa marudiano ugenini Kampala wakati nyumbani walipata ushindi wa magoli 2-1.