Mtwara. Ubovu wa uwanja wa Makonga, umetajwa kuwa sababu iliyowafanya Ruvu Shooting kufungwa kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Tandahimba.
Ruvu Shooting wamepoteza mchezo huo wa kirafiki kwa mabao 2-1 mbele ya wanachama wao wapya 183.
Kocha wa maafande hao, Abdulmutik Haji. alisema vijana wake walishindwa kuendana na ubovu wa uwanja huo.
"Vijana walicheza vizuri lakini tatizo lililotufanya kutoonyesha ubora wetu kwa kiwango cha juu zaidi ni uwanja.
" Pasi zetu nyingi zilikuwa zikikwama njiani lakini tumepata mazoezi ya kutosha kutoka kwao nadhani kwa maandalizi haya, tutakuwa na msimu mzuri," alisema Haji.
Bao la Ruvu Shooting kwenye mchezo huo wa kirafiki lilifungwa na Fully Zully Maganga huku yale ya Tandahimba City yakifungwa na Sadati Mpochi.
Ruvu Shooting itauanza msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwa kucheza dhidi ya Ndanda kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Mabatini, Agosti 22.