BAADA ya kuisaidia DTB kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya African Lyon, mshambuliaji Amis Tambwe amesema ndoto yake ni kutwaa kiatu cha ufungaji bora katika michuano ya Championship baada ya kuwa mfungaji bora Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tambwe ameanza vyema kampeni ya kusaka kiatu cha ufungaji baada ya kufunga mabao manne na kuisaidia DTB kupaa kileleni mwa msimamo wa Championship kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Tambwe alisema malengo yao ni kupanda Ligi Kuu msimu ujao lakini pia lengo lake ni kufunga mabao mengi zaidi ili aweze kuweka rekodi ya kuchukua kiatu cha ufungaji bora kama alivyofanya alipokuwa akicheza Ligi Kuu Tanzania Bara ambako alichukua mara mbili akiwa na Simba na Yanga.
"Ndoto yangu ilikuwa ni kuisaidia timu yangu kupata pointi tatu katika mchezo wetu wa kwanza ili tuanze mapema kutafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.”
"Malengo yangu ni kuwa mfungaji bora na hilo linawezekana kama tutaendelea kushirikiana. Huu ni mwanzo tu naamini kuna mengi mazuri yanakuja,” alisema Tambwe.
Kocha Mkuu wa DTB, Ramadhan Nsanzurwimo alisema ulikuwa mchezo mzuri na kuwashukuru wachezaji wake kwa ushindi huo.
Alisema hawezi kuwabeza wapinzani wake ila uzoefu uliwabeba baada ya kuwa mbele kwa mabao 4-1 vijana wake wakaridhika.
“Tulicheza na timu isiyokuwa na uzoefu, Tambwe alikuwa afunge mabao zaidi ya sita leo (juzi) lakini akafunga manne, yalikuwa matokeo mazuri tunamshukuru Mungu na tunajipanga na michezo ijayo,” alisema Nsanzurwimo.