Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru: Watazitapika fedha za JPM Afcon U-17

32979 Mwakyembe+pic Takukuru: Watazitapika fedha za JPM Afcon U-17

Tue, 19 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mwakyembe asema Rais wa TFF hawezi kujiweka kando, amtaka kutoa...

WAKATI Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), ikisema waliotafuna fedha zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli lazima wazitapike kama ambavyo alionya wakati akizitoa.

Rais Magufuli alitoa fedha hizo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U-17), yaliyofanyika nchini Aprili mwaka jana na wakati akitoa alionya endapo zitatumika ndivyo sivyo walaji watazitapika.

Hata hivyo, Takukuru imeeleza kulikuwa na upigaji katika fedha hizo, jambo ambalo imelifanya kuingia kazini kuchunguza huku ikiwataka waliozichota kuzirejesha mapema.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kupitia kituo kimoja cha redio nchini, Waziri Mwakyembe alisema TFF inapaswa kupeleka ushahidi Takukuru na si kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kujitetea na kwamba kwa kufanya hivyo si sahihi kwa sasa kwa sababu taasisi hiyo tayari imeanza uchunguzi.

Dk. Mwakyembe alisema katika sakata hili Karia hawezi kujiweka kando kwa kuwa yeye aliingia moja kwa moja katika kamati ya maandalizi ya ndani (Local Organizer Committee) za fainali hizo, hivyo kinachotakiwa kwake na shirikisho hilo ni kutoa ushirikiano kwa Takukuru ili iweze kufanya kazi yake.

Aidha, Dk. Mwakyembe alisema vyombo vya habari vinapaswa kuwa makini katika kuripoti suala hilo kwa kuwa hata fedha zinazochunguzwa si Sh. bilioni moja kama ambavyo vinaripoti kwa kuwa kiasi kilichopokelewa kilikuwa zaidi ya Sh. bilioni 1.7.

"Kuhusu hela msipotoshe mjadala zilikuwa zaidi ya Sh. bilioni 1.7, iacheni Takukuru ifanye kazi yake, wasaidieni Takukuru kama kuna kitu pelekeni huko, niwaombe wote hata BMT [Baraza la Michezo Tanzania] nao kama wana kitu wapeleke huko," alisema waziri huyo mwenye dhamana na michezo nchini.

Alisema mbali na Sh. bilioni moja iliyotolewa na Rais Magufuli, zipo fedha zingine kutoka kwa wadau mbalimbali waliochangia katika kufanikisha maandalizi ya michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini.

Alipoulizwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia John Mbungo, alisema bado wanaendelea na uchunguzi na taasisi hiyo haitabakiza kitu na kwamba waliozitafuna lazima wazitapike kama ambavyo Rais Magufuli alitamka wakati akizitoa.

"Bado tupo kwenye uchunguzi, tuacheni kwanza kwa sababu kwa sasa kila mtu ataongea chake, kila kitu lazima kichunguzwe, hatutabakisha kitu lazima wazitapike kama ambavyo rais alisema, sisi tumewaagiza wazirudishe hizo fedha," alisema.

Kadhalika, Mbungo naye alieleza fedha zinazochunguzwa ni zaidi ya Sh. bilioni moja kwa kuwa wapo wadau mbalimbali walitoa michango yao ili kufanikisha fainali hizo likiwamo Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Wiki iliyopita Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alisema fedha hizo zilikuwa chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya ndani ambaye alikuwa Waziri Mwakyembe na makamu wake, Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga.

"Fedha kupokelewa na matumizi yake, yalikuwa yanasimamiwa na vyombo vinavyohusika na wizara yenye dhamana ya michezo, sisi kama TFF, fedha hatukupata kupitia kwetu, zilipitia katika mamlaka nyingine ili kufanikisha mashindano yanayofanyika," alisema Kidao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live