Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars sasa washindwe wenyewe

74359 Stars+pic

Thu, 5 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bujumbura, Burundi. SULUHU katika mechi ya marudiano Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam itatosha kuipeleka Taifa Stars kwenye hatua ya makundi ya mchujo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 baada ya jana kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Burundi.

Straika Simon Msuva alifunga goli muhimu la kusawazisha zikiwa zimesalia dakika tano baada ya wenyeji kupata goli la kuongoza katika dakika ya 81 kupitia kwa Amissi Cedric.

Sare hiyo ilimaanisha kwamba Stars inahitaji japo sare ya 0-0 ama ushindi wowote ili kusonga mbele katika hatua ya makundi, ambayo itajumuisha timu 40 za Afrika zitakazogawanywa katika makundi 10 ya timu nne-nne. Sare ya mabao zaidi ya moja itaong’oa Stars kwa faida ya mabao ya ugenini.

Katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Intwari jijini hapa, Burundi walitangulia kupata bao lilitokana na beki Haruna Shamte kushindwa kumzuia winga wa Burundi ambaye alikimbia mpaka nje ya boksi na kuwapiga chenga mabeki Erasto Nyoni na Kelvin Yondani, kabla ya kumpasia Cedric ndani ya 18 aliyefumua shuti lililopita jirani na nguzo aliyokuwa amebana kipa Juma Kaseja.

Kabla ya Burundi kupata bao hilo, Saimon Msuva alishindwa kutumia vyema nafasi ya kufunga bao dakika ya 17 baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa Jonathan Nahimana.

Msuva alipokea pasi nzuri kutoka kwa Salum Abubakar na akiwa anatazamana na Nahimana alipiga shuti lililopanguliwa na kipa huyo na kushindwa kuipatia Stars bao la kuongoza.

Pia Soma

Advertisement
Katika kipindi cha pili, Stars walianza kwa kuonyesha kuhitaji goli na katika dakika 55 ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Hassan Dilunga na kuingia Idd Seleman ‘Idd Nado’ ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.

Stars ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Salum Abubakar na nafasi yake ilichukuliwa na Frank Domayo.

Katika dakika 85, Msuva alisawazisha bao baada ya Yondani kupiga pasi ndefu iliyowachanganya mabeki wa Burundi na kipa wao Nahimana, na mpira huo kuangukia katika njia ya Msuva aliyepiga shuti ulioenda moja kwa moja wavuni ukichungwa na Mbwana Samatta aliyeutumia vyema mwili wake kumzuia beki wa Burundi aliyekuwa akikaribia kuuokoa juu ya mstari wa goli.

Chanzo: mwananchi.co.tz