Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TUONGEE KIUME: Bei ya chee ya ving’amuzi imeharibu kombe la dunia

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unakumbuka kipindi ving’amuzi vilivyokuwa ni kitu cha anasa? Yaani ili uwe nacho ni lazima uwe umeangamiza kikatili akaunti yako ya benki kama sio kupondaponda na kuteketeza vibubu kibao au kujitwisha bonge la mkopo ambalo unaweza kuhenya kuulipa kwa mwaka mzima na miezi miwili ya mwaka unaofuatia — kile ndiyo kilikuwa kipindi kinachokuja na misimu ya kombe la dunia lenye utamu wake.

Mpira umebaki bado, japo ni tofauti mno na ule wa zamani. Lakini kwa wapenzi wa soka bado burudani wanaiona— vitu havijabadilika sana. Wachezaji wakali wapo, magoli matamu mengi sana, vyenga ndio usiseme, mastori ya nje ya uwanja, utani wa jadi na vita vya kisoka vya ukweli viko palepale— sana tu.

Lakini shida na mateso wanaipata wavimba macho. Watu ambao wanashabikia timu zote za zinazocheza kombe la dunia. Kuanzia Saudi Arabia, Nigeria hadi Ureno. Hawa wenyewe hawafahamu kuhusu kinachoendelea kwenye kombe la dunia, au kama wanaelewa na kufahamu ni kwa mbali sana. Lakini zaidi, taaluma na talanta yao ni kuteleza na fursa zinazopatikana kupitia kombe la dunia.

Wenyewe enzi zile za ugumu wa kumiliki ving’amuzi wao walikuwa wanatembea na reli ya ‘world cup’ tu. Wanatumia kama upenyo wa kuchomoka nyumbani kwenye kufuatilia makombe ya dunia wanayoyafahamu wenyewe — ukiaga kwa mama watoto unakwenda kutazama mechi ya Brazili dhidi ya Uruguay unadhani anaweza kuwa na pingamizi? Atake asitake, atataka tu kukuruhusu uende.

Utaenda kwenye kombe la dunia lako. Na likiisha, haraka utatafuta matokeo ya kombe la dunia la duniani na stori mbili tatu za uongo na kweli ili ukirudi nyumbani, mke akusikie tangu ukiwa njiani unavyobishana kuhusu Messi na Argentina yake kung’oka mapema. Hapo utapiga porojo kibao, maneno mengi kama dalali wa vyumba vya mabondeni.

Ukiingia nyumbani, mwepesi, mke anajua umetoka kwenye soka na wenzako. Kumbe umetoka kwenye soka lako unalolijua mwenyewe. Watu wamecheza sana hii michezo.

Lakini sasa hivi ni mateso kwa wavimba macho. Siku hizi hakuna kwenda kuangalia kombe la dunia nje ya nyumbani labda uwe mbabe. Huwezi kwenda kwa sababu ving’amuzi vimekuwa bei chee kushinda hata runinga zenyewe. Ukiwa na hata 30,000 unaweza ukacheki ‘game’ ukiwa sebuleni kwako na mama watoto anakuandalia msosi wa jioni unausikia unavyonukia.

Kwa mashabiki wa soka wa kweli hii inaweza kuwa ahueni. Lakini kwa wazee wa kazi, wazee wa kucheza na fursa, hii ya kupungua bei za ving’amuzi ni janga kubwa zaidi ya ambavyo mtu wa kawaida anaweza kufikiria. Watapata tabu sana.

Chanzo: mwananchi.co.tz