Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TOC yaonya wanamichezo Olimpiki

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya Afrika kutengewa Dola1 milioni  (Sh 2.2 bilioni) za maandalizi kwa ajili ya Olimpiki ya 2020 nchini Japan, Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), imesema kama wanamichezo wa Tanzania hawatofikia viwango ambavyo vimeweka, itakuwa ndoto kupata mgao wa fedha hizo.

Hivi karibuni, Chama cha Kamati ya Olimpiki Afrika (ANOCA) kilitangaza kutenga fedha hizo kwa ajili ya maandalizi ya timu za riadha, judo, kunyanyua vitu vizito, ngumi, tenisi na kuogelea kwa ajili ya Olimpiki ya 2020 itakayofanyika nchini Japan.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema kama wanamichezo wa Tanzania hawatokuwa kwenye viwango ambavyo ANOCA imeweka basi ni ndoto kupata fungu hilo.

"ANOCA inataka mchezaji ambaye ataandaliwa kwa kutumia fedha hizo awe ni namba tatu kwa ubora Afrika na namba 10 wa dunia, kinyume na hapo fedha hizo tutazisikia tu," alisema Bayi.

Alisema ANOCA imejikita katika maandalizi ili kuongeza idadi ya medali kwa Afrika kwenye Olimpiki ya 2020 baada ya ile ya 2016 nchini Brazil, Afrika kutwaa medali 45 pekee.

Wakati huo huo, ANOCA imetoa msimamo kuwa kiongozi atakayeruhusiwa kuongoza kamisheni ya wachezaji anapaswa kuwa ameshiriki Olimpiki kwa misimu mitatu.

Msimamo huo wa ANOCA unawaweka njia panda wanamichezo wa Tanzania ambao awali Tanzania ilikuwa ikitoa nafasi kwa wanamichezo waliowahi kushiriki michezo ya Afrika (All Afrika games) na Jumuiya ya madola pia kuongoza kamisheni hiyo ambayo inafanya uchaguzi kila baada ya miaka minne na uchaguzi ujao utafanyika 2020.

"Watakaoruhusiwa sasa kugombea kwenye uchaguzi wa Kamisheni ya 2020 ni wanamichezo walioshiriki Olimpiki kati ya 2012 nchini Uingereza, 2016 nchini Brazil au ile ya 2020 nchini Japan, kinyume na hao hatoruhusiwa kugombea kwenye Athlete Comission, kamisheni hiyo iliongozwa na wale walioshiriki michezo kwani pia wameweka muda wa kugombea kwenye kamati ya wachezaji," alisema Bayi.

Wanamichezo wenye nafasi hiyo sasa ni wanariadha, Faustine Mussa, Zakia Mrisho, Fabiano Joseph, Said Makula, Sarah Ramadhan na Alphonce Simbu, mchezaji judo, Andrew Thomas, bondia Suleiman Kidunda na waogeleaji, Magdalena Mosha na Hilal Hilal.



Chanzo: mwananchi.co.tz