Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TOC yanusuru riadha taifa

1371edc9fd1ced3f9bcfc2f0a89bdd91.png TOC yanusuru riadha taifa

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BAADA ya kutofanyika kwa mashindano ya taifa ya riadha kwa miaka mitano, Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imetoa Sh milioni 45 kuhakikisha yanafanyika kuanzia Septemba 12 hadi 13.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zalla alisema jana kuwa mashindano hayo kwa mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2015 katika Viwanja vya Shule za Filbert Bayi Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.

Alisema kuwa RT walikuwa wakiendesha mashindano ya wazi, lakini mwaka huu anaishukuru TOC kwa kusaidia kufanyika kwa mashindano hayo, ambayo yatashirikisha wanariadha wote nyota.

Alisema mwanariadha yeyote nyota ambaye atashindwa kushiriki mashindano hayo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu, kwani mashindano hayo yatatumika kupata wale watakaokwenda kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi, jumla ya wanariadha 213 na makocha 36 watashiriki mashindano hayo, ambayo TOC itagharamia malazi, chakula, namba, fulana kwa wachezaji na makocha wao pamoja na sare za waamuzi.

Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau alisema mashindano hayo, ambayo awali yalitakiwa kufanyika Septemba 5-6 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa), yameahirishwa baada ya Chuo Kikuu cha Elimu (Duce), ambako wachezaji wangefikia, watakuwa wakimalizia mitihani yao.

Alisema ili kuondoa mkanganyiko, wameamua kuyasogeza mbele kwa wiki moja na sasa yatafanyika Septemba 12 na 13.

Zavalla aliishukuru TOC kwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mashindano hayo, ambayo hayajafanyika kwa miaka mingi.

TOC imekuwa ikisaidia michezo mbalimbali, ambapo hivi karibuni ililipiga jeki Shirikisho la Ndondi za Wazi Tanzania (OBFT) mabobdia wake kwenda katika mashindano ya Afrika kusaka nafasi ya kufuzu kwa Olimpiki 2020, lakini walishindwa.

Chanzo: habarileo.co.tz