Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFF yarushiana mpira suala la Nchimbi

90409 Nchimbi+pic TFF yarushiana mpira suala la Nchimbi

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Matumaini ya Yanga kumtumia Ditram Nchimbi dhidi ya Simba, yapo shakani baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuzuia leseni yake.

Uamuzi wa TFF unaiweka Yanga katika mazingira magumu ya kumtumia kwa kuwa zimebaki siku chache kabla ya timu hiyo kuvaana na watani wake wa jadi Simba, Jumamosi wiki hii.

Yanga ilimuombea leseni Nchimbi na wachezaji wengine Adeyun Saleh na Taliq Seif ili kuwatumia katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mujibu wa taratibu na sheria. Adeyun na Taliq wamepata leseni.

Nchimbi amesajiliwa na Yanga akitokea Azam ingawa ameibua sintofahamu baada ya Polisi Tanzania alikokuwa akicheza kwa mkopo kuweka pingamizi TFF.

Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alidai Nchimbi amezuiwa na klabu hiyo na wameitaka Yanga kuzungumza kufikia mwafaka.

“Hili jambo linatushangaza kwani mchezaji alikuwa mali ya Azam au Polisi Tanzamia? Hatujui mantiki ya TFF kuzuia leseni yake tulifuata taratibu zote za kumpata kutoka Azam,” alisema Bumbuli.

Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo ni Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi.

“Sina maelezo ya kina kuhusiana na suala hilo naomba uwasiliane na Kidifu (Herman) ambaye ataelezea suala hilo kisheria,” alisema Madadi.

Hata hivyo, Kidifu alipotakiwa kutoa tamko kuhusu usajili wa Nchimbi alisema anayepaswa kuzungumzia suala hilo ni Madadi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alisema wameweka pingamizi TFF kusajiliwa na Yanga kwa kuwa walimpa fedha anazotakiwa kurejesha ili zitumike kusajili mchezaji mwingine.

“Nchimbi anajua fedha tulizompa kutokana na makubaliano maalumu, hizi ni fedha za Serikali haziwezi kupotea lazima suala hili lijadiliwe kwa pande zote mbili. Hatuna nia ya kumtumia shida yetu ni fedha,” alisema Lukwaro.

Chanzo: mwananchi.co.tz