Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFF yapigilia msumari Yanga SC

50037 YANGA+PIC

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya uwepo wa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wanachama wawili wa Yanga kupinga uchaguzi wa klabu hiyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Ally Mchungahela alisema uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utafanyika Mei 5 badala ya Aprili 28 kama ilivyotangazwa awali na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Yanga, George Mkuchika.

Mchungahela alisema kuwa wamesogeza mbele uchaguzi huo kwa kuwa Aprili 28 itakuwa siku ya mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana (Afcon).

Mwenyekiti huyo alisema hawakushughulika na kesi iliyofunguliwa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam kwa madai kuwa haiwahusu.

“Kesi iliyofunguliwa ilikuwa ya kupinga kadi za benki kutumika katika uchaguzi na si kupinga uchaguzi, hivyo hilo halikuwa kwa TFF,” alisema Mchungahela.

Hata hivyo, wanachama wa klabu ya Yanga Juma Magoma na Athumani Nyumba walifungua kesi ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2019, kupinga kufanyika uchaguzi huo kwa madai unakwenda kinyume cha katiba ya klabu hiyo.

Katika madai yao Magoma na Nyumba wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai unakwenda kinyume cha katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010 ibara ya 7.

Ibara hiyo inaelezea utaratibu wa uanachama ndani ya Klabu ya Yanga ambao, kwanza ni kutuma maombi, ambapo maombi hayo yatapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, ambayo baadaye yatajadiliwa na Kamati ya Utendaji.

Pia, ibara hiyo, inaelezea kuwa maombi hayo yataambatana na fomu namba YASC/U, ada ya uanachama ambayo ni Sh 12,000 pamoja na ada ya kadi ambayo ni Sh 2,000.

Pia wanadai kuna taarifa za kuwepo wanachama wenye kadi feki za kieletroniki ambazo zina saini na mhuri zinazosambaa kwa baadhi ya wanachama, ambazo zinaonyesha zimetolewa na benki ya CRDB na Benki ya Posta.

Wanadai kadi hizo zinazodaiwa ni kadi za uanachama wa Klabu ya Yanga, zikiwa na picha za wamiliki ambazo sio mali ya klabu hiyo.

Magoma na Nyumba wanapinga matumizi ya kadi hizo wakidai kuwa kwa namna yoyote ile haziwezi kuwa uthibitisho wa uanachama wa Yanga, kwa kuzingatia kwamba, wahusika wa kadi hizo, hawakupitia utaratibu ulioanishwa katika ibara ya 7 ya mwaka 2010 ya Katiba ya Yanga.

Pia Mchungahela alisema anatarajia uchaguzi huo utafanyika kwa uhuru baada ya wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji kujiuzulu kupisha mchakato huo.

“Tunawaacha Wanayanga kufanya uchaguzi kwa uhuru, ndio maana viongozi wao walijiuzulu ili kupisha zoezi hilo, hata fomu tumeacha zichukuliwe kwenye klabu yao kuanzia leo (jana) Jumanne.

“Ambao watafanya uchaguzi ni wale ambao wapo kwenye kitabu cha leja ndio maana leja ya Yanga tumepewa TFF kwa ajili ya kushirikiana nao katika jambo hilo,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, Samuel Mapande alisema wamekubaliana na TFF kufanyika uchaguzi huo.

“TFF watasimamia kama mamlaka iliyopo juu yetu lakini Wanayanga watakuwa huru na kuendesha taratibu zote zinazotakiwa kwa mujibu wa Katiba ya klabu yetu,” alisema Mapande.



Chanzo: mwananchi.co.tz