Dar es Salaam. Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetoa baraka kwa Kamati ya Uchaguzi ya Simba kuendelea na mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Klabu hiyo utakaofanyika Novemba 3, mwaka huu.
Uamuzi huo ni hitimisho la hofu iliyoanza kutanda kwa wanachama wa Simba na wadau wa soka nchini juu ya kufutwa uchaguzi huo kutokana na kile kilichodaiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kukiukwa kwa baadhi ya kanuni na utaratibu wa uchaguzi wa shirikisho hilo ambalo Simba ni mwanachama wake.
Septemba 17, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Revocatus Kuuli alisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Simba kwa madai ya kutofuatwa kwa baadhi ya utaratibu na kanuni za uchaguzi.
“Tumewapa taarifa ya kusimamisha mchakato huo na chochote kitachofanyika bila kufuata maelekezo yetu ni batili. Bado wana nafasi ya kurekebisha wakishirikiana na kamati yetu. Huo ni utaratibu kwa klabu yoyote ambayo ni mwanachama wa TFF,” alisema Wakili Kuuli.
Akizungumza na gazeti hili jana, Wakili Kuuli alisema hakuna tatizo kwa Simba kuendelea na mchakato huo kwa kuwa wametimiza kwa ufasaha maelekezo ambayo walipewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
“Kamati yetu haikusimamisha uchaguzi wote bali kuna baadhi ya mambo walitakiwa kurekebisha ikiwemo suala la ada za fomu pamoja na kuishirikisha Kamati ya Uchaguzi ya TFF sambamba na kamati kama vile za rufani na maadili za shirikisho. “Kwa bahati nzuri wameweza kutimiza masharti hayo tuliyowapa wanaweza kuendelea na mchakato kama kawaida. Kuhusu suala la wale ambao walishindwa kugombea kwa sababu ada ya fomu ilikuwa kubwa nadhani sasa wana nafasi ya kukata rufani muda ukifika,” alisema Wakili Kuuli.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Boniface Lyamwike alisema hakutakuwa na mabadiliko ya tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi au kupunguza siku za kampeni hadi kufikia tano kama TFF ilivyowataka mwanzoni. “Kuhusu suala gharama la ada za fomu za kuwania fomu, kiwango kilichowekwa na kamati hakikuwa na tatizo lolote, lakini pia hata hili la urefu wa muda wa kampeni hakuna kifungu chochote hata kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF kinachozuia muda wa kufanya kampeni kuwa siku 30.
Kilichokuwepo ni mazoea tu lakini hilo la kushirikisha Kamati za TFF tumelifanyia kazi ingawa muda wa kampeni kiuhalisia utapungua kwa sababu kuna utaratibu wa kukata rufani na kuweka mapingamizi ambao tumeingiza kwenye mchakato hivyo moja kwa moja muda wa kampeni utapungua,” alisema Lyanwike.
Wanachama 19 walichukua fomu kuwania Mtemi Ramadhani na Swedi Nkwabi waliwania uenyekiti na wadau waliochukua fomu kugombea ujumbe ni Christopher Mwansasu, Dokta Zawadi Ally Kadunda, Abubakar Zebo, Patrick Rweyemamu, Hamisi Mkoma, Ally Suru, Alfred Eliya na Omari Selemani.
Wengine ni Mohamed Wandi, Juma Pinto, Said Tully, Mwina Kaduguda, Idd Kajuna, Hussein Mlinga, Jasmeen Badou na Asha Baraka.