Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF kupitia kwa afisa habari wake, Clifford Mario Ndimbo limetoa ufafanuzi juu ya hatma ya klabu ya Mtibwa Sugar kushiriki michuano ya kimataifa endapo itashinda taji la Kombe la Shirikisho hapo kesho dhidi ya Singida United.
Kupitia mahojiano yake na kituo cha radio ya EFM, Ndimbo amesema kuwa mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu soka Tanzania Bara timu ya Mtibwa Sugar inayo nafasi ya kushiriki michuano ya CAF endapo itaibuka na ushindi kwakuwa adhabu yake ya miaka mitatu imemalizika na kama kutakuwa na tofauti yoyote kutoka Shirikisho la soka barani Afrika watajua chakufanya.
Baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu mwaka 2000 klabu ya Mtibwa Sugar ilishindwa kusafirisha timu kushiriki michuano ya kimataifa kufuatia ukata wa fedha na ndipo Shirikisho la soka barani Afrika ikaipatia adhabu ya kuifungia miaka mitatu kutoshiriki michuano ya CAF.
Hapo kesho siku ya Jumamosi Mtibwa itashuka dimbani kuikabili Singida United katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuwania nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Shirikisho.