Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TEF, MCT na Tamwa wawalilia wafanyakazi Azam Tv

66035 MCT+PIC

Mon, 8 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa habari nchini Tanzania, wameendelea kuwalilia wanahabari watano wa kampuni ya Azam Limited waliofariki dunia kwenye ajali mkoani Singida.

Ajali hiyo imetokea leo Jumatatu Julai 8,2019 eneo Shelui mkoani humo Singida, Tanzania na imeua watu saba wakiwemo wafanyakazi hao baada ya gari waliokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori wakati wakielekea Chato mkoani Geita katika uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Chato-Burigi.

Wadau hao ni pamoja Baraza la Habari Tanzania (MCT), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Mkurugenzi wa Tamwa, Rose Reuben amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo za wanahabari hao vijana na kusema Taifa limepoteza nguvu kazi.

 “Msiba huu ni mkubwa kwa tasnia ya habari Tanzania. Tamwa inaungana na Watanzania wote kutoa pole kwa uongozi wa Azam Media Group, mkurugenzi wa Azam televisheni Tido Mhando.”

“Vifo hivi vimeacha pengo kubwa kwa wana tasnia ya habari, kwa sababu wamefariki wakitimiza majukumu yao. Mungu azilaze roho za marehemu peponi na awajalie unafuu wa haraka majeruhi,” amesema Reuben.

Pia Soma

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga ameungana na Reuben kutoa pole kwa uongozi wa Azam akisema ajali hiyo ni tukio baya lililokatisha maisha ya wachapa kazi hodari kwenye kampuni hiyo.

Mukajanga amesema ajali hiyo imeleta majonzi makubwa kwa kuwa wanahabari walikuwa kwenye harakati za kutimiza majukumu yao kwa lengo la kuwapasha habari Watanzania na dunia.

 

“Juni 29 mwaka huu katika kilele cha Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (Ejat)2018 zilizoandaliwa na MCT na washirika wake, mmoja wa wafanyakazi waliofariki alipanda jukwaani na kutunukiwa katika kundi la Utalii na Uhifadhi upande wa runinga.

“Tunachukua fursa hii kutoa pole za dhati na rambirambi kwa uongozi  na wafanyakazi wa Azam kwa kufikwa na msiba huu mzito,” amesema Mukajanga.

Katibu wa TEF Neville Meena amesema jukwaa hilo linaungana na wanatasnia wote wa habari nchini kutoa pole kwa uongozi, menejimenti na wafanyakazi wote wa Azam kutokana msiba huo.

 “TEF tumehuzunishwa, kusikitishwa na kuumizwa na msiba huu kwani tasnia imewapoteza wafanyakazi na wanataaluma mahiri ambao walikuwa wakielekea Chato mkoani Geita kutimiza majukumu yao.

“Ajali hii imeacha simanzi kubwa kwa tasnia ya habari na wanahabari kwa ujumla.Hili ni pigo kubwa kwa taaluma ya habari nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz