Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven ni noma, mbele wembe ukuta chuma

90292 Sven+pic Sven ni noma, mbele wembe ukuta chuma

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha mpya wa Simba, Sven Ludwig Vandenbroek ameendeleza mwanzo mzuri klabuni hapo kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana na kuandika rekodi ya kuvutia katika mechi zake za kwanza Msimbazi.

Katika mechi zake tatu za kwanza za michuano yote, Mbelgiji huyo aliyechukua kiti cha Mbelgiji mwenzake, Patrick Aussems aliyetupiwa virago, ameiongoza Simba kufunga mabao 12 bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa.

Winga Mcongo, Deo Kanda aliifungia Simba bao la kuongoza katika dakika ya kwanza ya kipindi cha pili akiunganisha vyema krosi ya Hassan Dilunga kutokea wingi ya kulia na Mbrazili Gerson Fraga akahitimisha ushindi wa kujiamini kwa shuti shuti la chini lililopita jirani na nguzo ya lango katika dakika za lalasalama.

Ushindi uliimarisha Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 31 baada ya mechi 12.

Ulikuwa ni ushindi wa tatu mfululizo wa kocha Sven ambaye awali aliiongoza Simba kushinda 6-0 dhidi ya AFC Arusha katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka la Tanzania Bara na kisha kuifunga Lipuli ya Iringa kwa mabao 4-0 katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Bara.

Mabingwa mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu Bara Simba wako pointi saba juu ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 24 na imecheza mechi moja zaidi ya Simba.

Yanga ilipaa juzi kutoka nafasi ya tisa hadi kuingia ndani ya 3-Bora kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons mjini Iringa. Wana Jangwani wana pointi 21 baada ya mechi 10.

Simba itacheza mechi ijayo dhidi ya Ndanda keshokutwa Jumanne, wakati Yanga itawavaa Biashara United kesho Jumatatu.

Baada ya mechi hizo, Simba na Yanga zitakutana katika mechi ya wapinzani wa jadi itakayopigwa Januari kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 20 baada ya mechi 11, itaikabili Polisi Tanzania jioni ya leo kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi.

Timu hizo zinakutana zikitokea kupata matokeo tofauti katika mechi zao zilizotangulia. Azam walilala 1-0 jijini Tanga mbele ya Wagosi wa Kaya, wakati maafande walitakata nyumbani kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya KMC.

Kutokana na matokeo hayo, timu zote zimeupania mchezo wa leo, huku Azam wakisisitiza hawatakubali kulala tena ugenini, huku wenyeji wanaonolewa na Kocha Malale Hamsini wakisisitiza dozi inaendelea kama kawaida ili kuhakikisha wanamaliza msimu katika nafasi nzuri.

Azam haijapata matokeo mazuri katika michezo yake miwili mfululizo. Ilianza kutoka sare ya 2-2 dhidi ya JKT Tanzania kisha ikachapwa 1-0 na Coastal, hivyo kocha msaidizi wa kikosi hicho, Idd Nassor ‘Cheche’ amesema sasa imetosha.

Cheche alisema wameyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal na wanaingia kuikabili Polisi kwa nguvu zote kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu.

“Polisi Tanzania ni wazuri na tunawaheshimu, na tunajua wako nyumbani, lakini tutahakikisha tunapambana kwa hali zote ili tuweze kupata matokeo mazuri,” alisema Cheche.

Kocha wa Polisi, Malale alisema: “Tunajua tunakutana na timu iliyotoka kupoteza mechi hivyo watakuja kwetu wakihitaji kupata matokeo mazuri kupitia sisi. Tunajua itakuwa mechi yenye ushindani mkubwa lakini tumejipanga kuwakabili.”

Chanzo: mwananchi.co.tz