Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven kaja kipindi kibaya, ila Jangwani wasichekelee

88759 Kocha+pic Sven kaja kipindi kibaya, ila Jangwani wasichekelee

Tue, 17 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

LIGI Kuu Bara imesimama kwa muda, kupisha michuano ya Kombe la Chalenji 2019 inayofanyika Uganda. Hata hivyo tayari Bodi ya Ligi (TPLB) kama kawaida wameshafanya yao. Wametangaza ratiba mpya ikizijumuisha Simba na Yanga.

Awali Simba na Yanga zilikuwa zimepewa shushuu mpaka Januari 4 zitakapokutana katika pambano la kwanza la watani msimu huu.

Lakini sasa, Yanga inapaswa kupanga mabegi yake mara baada ya mechi yao ya Kombe la FA dhidi ya Iringa United, kwa ajili ya safari ya kwenda jijini Mbeya. Kule watakuwa na mechi mbili mfululizo dhidi ya Mbeya City kabla ya kumalizana na wababe wasiofungika wa Tanzania Prisons.

Baada ya mechi hizo watarudi Dar kupepetana na Biashara United ndipo siku chache zinazosalia wajiandae dhidi ya Simba ambao ratiba inaonyesha watacheza mechi nne mfululizo nyumbani kama wenyeji. Inashangaza kidogo! Itaanza na Lipuli, kisha KMC na kumalizana na Ndanda kabla ya kuvaana na Yanga katika mechi ya watani. Yanga walishaanza kupiga kelele, lakini ni kama zile za chura tu, hazimzuii ng’ombe kunywa maji bwawani.

Binafsi nimependa ratiba hiyo, hata kama ina dosari ya timu moja kucheza mfululizo nyumbani, ila ile kasumba kwamba pambano la watani ni lazima Simba na Yanga zikaweke kambi ya wiki kadhaa, safari hii siioni, labda TBPL ije ifanye maajabu yake tena!

Ndio, TPLB huwa haitabiriki, leo inaweza kuamka hivi kesho ikaja kivingine, hivyo sio ajabu utakaposikia pambano la watani limeota mbawa Januari 4 na kupelekwa mbele. Kuna mambo katika soka huwa yanatokea Tanzania tu!

Simba na Yanga zitakutana zote zikiwa na makocha tofauti na wale walioanza nao msimu huu na waliokuwa nao zilipokutana mara ya mwisho Febuari 16 mwaka huu katika msimu uliopita.

Yanga ilianza kuachana na Mwinyi Zahera ambaye hajawahi kuonja ushindi wowote mbele ya Simba tangu atue Jangwani akimpokea mikoba George Lwandamina aliyekimbizwa na njaa!

Simba nao wamepeana mkono wa kwaheri na Patrick Aussems na tayari imeshamleta Kocha Mkuu mpya naye kutoka Ubelgiji, Sven Vanderbroek atakayesaidiana na Seleman Matola!

Matola ametua Msimbazi siku chache kabla ya VanderBroek akichukua nafasi ya Dennis Kitambi aliyekuwa msaidizi wa Aussems ambaye naye alitimuliwa klabuni hapo.

Matola ni kocha mzoefu ndani ya Simba na hasa kwenye mechi hizi za watani, kwani ameichezea na kuinoa Simba kwa siku za nyuma.

Jangwani nako kwa sasa inaye Charles Boniface Mkwasa kama kocha wa muda, lakini ikielezwa inafanya mchakato wa kimya kimya kupata Kocha Mkuu mpya wa kushika nafasi ya Zahera.

Katikati ya kuelekea kwenye pambano hilo la watani, dirisha dogo la usajili nalo litakuwa wazi, kwani linafunguliwa kuanzia kesho Jumatatu! Tayari baadhi ya klabu ikiwamo Yanga wameshaanza mambo, hasa ikizingatiwa, imeshawatema nyota wao wawili kwa mpigo, Juma Balinya na Sadney Urikhob waliosajiliwa msimu huu.

Yanga imemsajili Tariq Seif aliyewahi kutamba na Geita Gold, Stand United na Biashara United, japo kwa sasa anatokea Misri alikoenda kucheza soka la kulipwa mapema msimu huu.

Tariq inaelezwa ametua Jangwani ili kuziba nafasi za kina Sadney na Balinya Mfungaji na Mchezaji Bora wa Uganda kwa msimu uliopita, ambaye alishindwa kung’ara akiwa kikosi cha Yanga.

Wachezaji hao inaelezwa waliombwa kuachwa na Yanga kwa madai ya kushindwa kuvumilia njaa iliyopo Jangwani. Kuishi miezi miwili mfululizo bila mishahara kwao ilikuwa tabu kidogo.

Lamine Moro aliyeonekana kuiva na Kelvin Yondani na kuunda ukuta wa chuma Jangwani, naye inadaiwa ameomba pia kuachwa, lakini mabosi wa Yanga wanambembeleza arudi kupiga kazi!

Bila ya shaka wanachama na mashabiki wa Yanga, watakuwa na hamu ya kuona chama lao litafanya nini kwanza kwenye mechi zao tatu za awali kabla ya kuvaana na watani wao. Katika mechi yao ya mwisho ya Ligi msimu huu walitoka sare ya 1-1 dhidi ya KMC. Mbeya City sio wazuri msimu huu, lakini wanaisumbua sana Yanga wakiwa Mbeya na utamu imemnasa Amri Said aliyeiabisha Yanga msimu uliopita mjini Musoma alipokuwa Biashara United! Prisons msimu huu ni moto. Ndio timu pekee haijapoteza mchezo mpaka sasa katika ligi hiyo na Biashara wameonekana kuamka safari hii! Hivyo Yanga inapaswa kukaza mzuri kwelikweli kama inataka kwenda kwenye pambano la watani wakiwa na morali!

Upande wa Simba mechi dhidi ya Lipuli ndiyo pekee inayoonekana kuwa ngumu, ila zilizosalia kwa kuangalia nguvu za wapinzani wao, huenda ikapata mchekea, japo mpira unadunda.

Hata hivyo, Simba ipo chini ya makocha wapya ambao mechi hizo tatu ndizo zitakuwa kipimo kwao kabla ya kuvaana na Yanga. Sven Vanderbroek na Seleman Matola hawana siku nyingi tangu wasainishwe mikataba na kuanza kazi Msimbazi.

Kwa mazingira hayo kwa timu zote ni wazi safari hii pambano la watani linaweza kuwa matokeo yasiyotabirika na sura ya kipekee na pengine nyingine tofauti na mapambano yaliyopita tangu 1965.

Hivyo, kuanzia viongozi, makocha, wachezaji hadi wanachama na mashabiki ni wazi waelekeze nguvu zaidi kwenye mechi zao tatu za awali kabla ya pambano hilo la watani.

Naamini matokeo ya aina yoyote kwa mechi hizo za awali itatoa utabiri wa kitu gani kinachoweza kutokea Januari 4 kwa timu hizo.

Kuna wanaoamini huenda Yanga inaweza kutaabika kutokana na hali waliyonayo sasa, lakini ukweli hata Simba bado haina uhakika wa kuitambia Yanga Taifa kwa historia ya michezo ya watani.

Kipindi ambacho Simba ilionekana kuwa dhaifu ndipo walipokuwa wakipata matokeo ya kibabe dhidi ya Yanga na ile msimu iliyoonekana kuwa imara zaidi, ndipo walipotaabika Jangwani.

Ukweli ulivyo ni kwamba pambano la Simba na Yanga huwa lina mambo mengi ndani na nje ya uwanja, kitu muhimu ni kusubiri kuja kuona kipi kitakachotokea kwenye mchezo huo wa Janurai 4.

Lakini hii ni mechi mbaya zaidi kwa Simba ya Sven kama itapata matokeo mabaya mbele ya Yanga, kwa sababu baadhi ya mashabiki wa Msimbazi bado hawajui kwa nini Aussems alitimuliwa.

Kama Simba itapata matokeo mazuri itakuwa salama ya Sven na hata uongozi kwa ujumla, lakini vinginevyo inaweza kuwa mwanzo wa safari ya kurudi kwa Sven kwao na kusakamwa kwa viongozi.

Mechi hizo za Simba na Yanga mara nyingi, ndizo zinazoamua hatma ya makocha, hivyo Sven ni kama kama kipindi kibaya, lakini bado Jangwani hawapaswi kushangilia kwani nao wa msala wao!

Chanzo: mwananchi.co.tz