Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven amewasikia, sasa mtamkoma!

90007 Sven+pic Sven amewasikia, sasa mtamkoma!

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

SIKU moja mara ya Simba kumtambulisha kocha mkuu wao, Mbelgiji Sven Vandenbroek baadhi ya wadau waliibuka na kuponda wasifu wake wakidai hatishi kama watangulizi wake, kwa maana ya Pierre Lechantre na Patrick Aussems aliyepishana nao.

Hata hivyo, kumbe Sven amesikia kejeli zote za watu wanaomponda na kuwajibu kwa kuwaambia watulie tu na wenyewe ndio watakaogeuka kumshangilia kwa kile alichopania kukifanya ndani ya Simba.

Kocha huyo ambaye jana alikuwa akiiongoza Simba kwa mara ya pili katika mechi za mashindano tangu ale shavu Msimbazi, baada ya awali kushinda 6-0 katika Kombe la FA dhidi ya AFC Arusha, aliliambia Mwanaspoti hana wasiwasi na wasifu wake na amekuja kufanya vitu vikubwa.

Sven alisema kabla ya kukubaliwa kuanza kazi Simba alikutana na swali kama hilo juu ya wasifu wake kutoka kwa mabosi wake, lakini aliwajibu anakuja kufanya mambo mazuri katika timu hiyo na kutengeneza ukubwa wa jina lake pamoja na wasifu kupitia michuano watakayoshiriki.

“Malengo niliyojiwekea nikiwa hapa Simba naamini nitayafikia kwa kufanya wasifu wangu kuwa mkubwa kama makocha wengine ambao wamekuwa wakiwataja, kwa maana hiyo sina wasiwasi na naendelea na majukumu yangu,” alisema Sven mwenye miaka 40.

“Malengo yangu binafsi ni kuona Simba inachukua mataji mengi ya ndani kwa muda nitakaokuwepo hapa, lakini kufika mbali katika mashindano makubwa ya Afrika kama Ligi ya Mabingwa jambo ambalo uongozi wangu unatamani kuona tunalifikia hilo.

“Binafsi nina kiu ya kufanya vizuri hapa Simba na kuisaidia timu kufikia malengo kuwa miongoni mwa klabu kubwa kwani jambo hilo pia kwa upande wangu litatengeneza ukubwa wa jina langu na kufahamika.

“Kushindwa kukaa katika timu zaidi ya mwaka mmoja hilo linaweza kutokea katika majukumu yoyote, lakini kwa hapa Simba nadhani mambo yatakuwa tofauti kutokana na kuaminiwa na uongozi na ushirikiano nitakaopata naamini nitakaa kwa muda mrefu na kutengeneza timu imara.”

Wasifu wa Sven unaonyesha kuwa alianza kufundisha soka katika timu ya Niki Volou FC mwaka 2014, akiwa kama kocha msaidizi chini ya kocha mkuu Heverlee Leuven na baada ya hapo alikwenda kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Cameroon iliyokuwa chini ya kocha mkuu Hugo Broos, na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika 2017.

Baada ya hapo Julai 2018, alipata kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Zambia na ilipofika Februari 2019, Shirikisho la Soka la Zambia lilitangaza kuachana naye kutokana na kushindwa kufuzu katika fainali za mataifa Afrika (Afcon) zilizofanyika nchini Misri.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alinukuliwa akisema kigezo mojawapo kilichotumika kumpatia kazi Sven ni ujana alionao na kiu na njaa ya mafanikio makubwa aliyonayo.

“Hiyo kiu na njaa ya mafanikio ambayo anayo Sven ndio tunataka ailete kwetu ili kuona Simba inafanikiwa na hata mwenyewe atafaidika kwa kutengeneza wasifu wake, lakini tuliamua kuachana na makocha wakubwa kama Piere Lechantre, Milutin Sredejovic ‘Micho’ na wengineo kwanza gharama zao, lakini huenda wasiwe na jipya kutokana na mafanikio ambayo wameyapata katika timu mbalimbali,” alisema Senzo.

WA STARS KAZI WANAYO

Wachezaji saba waliokuwa kikosi cha taifa cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ katika mashindano ya Chalenji yaliyofanyika Uganda hivi karibuni kazi wanayo ya kumuonyesha Sven kuwa wanafaa kuingia katika kikosi cha kwanza kutokana na mazoezi mbalimbali ambayo wanaendelea kufanya tangu walipowasili Jumapili wiki iliyopita.

Sven alisema bado hajapata muda wa kutosha kuwaangalia wachezaji hao waliokuwa katika majukumu ya timu ya taifa kutokana na muda ambao walifanya mazoezi kuwa ni mfupi, lakini kabla ya dirisha la usajili kufungwa Januari 16 atakuwa ameona vitu vingi kutoka kwao.

“Hawa ambao nilianza nao kazi tangu nimefika hapa nimeona vitu vingi kwani kila mmoja ana uwezo wa kuingia katika kikosi cha kwanza, hata wale ambao hawakuwa wanatumika mara kwa mara, ila hawa waliokuwa Stars, wana kazi ya kujituma na kuonyesha walicho nacho,” alisema Sven.

“Nataka kuwaona wote pamoja kuwashindanisha ili kuongeza ushindani katika timu na kila ambaye anapata nafasi aende kujituma na kutimiza majukumu yake ipasavyo.”

Nyota hao wa Kilimanjaro Stars ni kipa Aishi Manula, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Gadiel Michael, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Jonas Mkude na Miraj Athumani.

Chanzo: mwananchi.co.tz