Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sudan yashika tiketi ya Stars Chalenji

88189 Cecafa+pic.png Sudan yashika tiketi ya Stars Chalenji

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

USHINDI wa bao 1-0 dhidi ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ ambao timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ iliupata juzi umekoleza vita baina yao na Sudan katika mashindano ya Chalenji yanayoendelea jijini hapa.

Matokeo hayo yameziweka timu zote tatu katika uwezekano wa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo itakayochezwa Jumanne, Disemba 17.

Baada ya Kenya kuwa timu ya kwanza kuingia hatua ya nusu fainali ikiongoza kundi B na pointi zake sita kutokana na kupata ushindi wa mechi mbili mfululizo, Zanzibar Heroes, Kilimanjaro Stars na Sudan kila moja inaweza kunyakua nafasi moja iliyobakia katika kundi hilo, ikiwa tu itachanga vyema karata zake katika mechi ya mwisho, Jumamosi, Disemba 14.

Kilimanjaro Stars ndio ipo kwenye nafasi nzuri zaidi kwani, ikiibuka na ushindi tu katika mchezo wa mwisho dhidi ya Sudan itafikisha pointi sita ambazo zitaipeleka nusu fainali ikiungana na Kenya.

Lakini, hata matokeo ya sare yanaweza kuibeba Stars kwani itafikisha pointi nne na ikiwa Zanzibar itafungwa au kutoka sare na Kenya, yenyewe itakuwa imefuzu.

Na hata ikitokea Stars ikatoka sare na Zanzibar Heroes ikapata ushindi dhidi ya Kenya, Stars inaweza kufuzu ikiwa itakuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kwani, hadi sasa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ilionao ni 0 wakati ndugu zao Zanzibar wana mabao -1.

Aina hiyo ya matokeo ambayo Stars wanayahitaji ili kusonga mbele ndio yameonekana kulipa nguvu benchi lake la ufundi ambalo limeahidi kufanya vizuri katika mchezo wa mwisho.

“Ni mechi ngumu dhidi ya Sudan kwani wote tuna nafasi ya kufuzu, lakini naamini tuko katika nafasi nzuri zaidi na tutajipanga kuhakikisha tunashinda ukizingatia kwamba, vijana molali iko juu baada ya ushindi dhidi ya Zanzibar,” alisema kocha Juma Mgunda wa Kilimanjaro Stars

Kwa Zanzibar wenyewe ambao wana pointi moja watakuwa na kibarua cha kuhakikisha wanaifunga Kenya katika mchezo wa mwisho na kuombea Kilimanjaro Stars ama ifungwe au itoke sare na Sudan.

Ikiwa hivyo maana yake Zanzibar Heroes itakuwa sawa kwa idadi ya pointi ama na Sudan au na Kilimanjaro Stars na hivyo timu itakayovuka kuamriwa kwa kuangalia kigezo cha utofauti wa mabao ya kufungwa na kufunga.

Sudan ambayo nayo ina pointi moja kama ilivyo kwa Zanzibar, utofauti wake wa mabao ya kufunga na kufungwa ni -1.

Kocha wa Zanzibar Heroes, Hemed Morocco alisema hakuna kinachoshindikana katika mchezo wa soka na bado wana matumaini ya kusonga mbele.

“Tunakwenda kufanyia kazi udhaifu tulioonyesha dhidi ya Kilimanjaro Stars ili tuweze kufanya vizuri tutakapokabiliana na Kenya.

Kimahesabu nafasi bado tunayo hivyo, hatuwezi kukata tamaa na tunawaomba mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi, lolote linaweza kutokea kwani huu ni mpira,” alisema Morocco.

Kwa upande wa Kocha wa Sudan, Elfatih Abubaker alisema bado wana matumaini ya kusonga mbele.

“Tuna pointi moja na kama tutashinda dhidi ya Tanzania, tutafikisha nne ambazo zinatosha kutupeleka hatua ya nusu fainali hivyo sidhani kama tunatakiwa kukata tamaa na badala yake ni kujipanga tuweze kupata ushindi katika mchezo wa mwisho.

Nafasi bado tunayo na jambo la msingi ni kupata ushindi kwanza kwenye mechi yetu na baada ya hapo kuangalia kitakachotokea katika hiyo mechi nyingine ingawa hata wenzetu Tanzania (Bara) na Zanzibar nao wana nafasi hiyo,” alisema Abubaker.

Chanzo: mwananchi.co.tz