Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars hii Ilikuwa lazima wapigwe tu!

48507 Stars++pic

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

UPANGAJI wa kikosi kilichoanza ulitoa picha ya wazi ya kuwa benchi la ufundi la Stars lilijua umuhimu wa kupata ushindi kwenye mchezo wa jana.

Tofauti na mechi zilizopita, kocha Emmanuel Amunike alianzisha kundi kubwa la wachezaji ambao, kiasili ni washambuliaji.

Makala hii inakuletea tathmini ya namna mchezaji mmoja mmoja wa Stars alivyotoa mchango katika mchezo wa jana.

Aishi Manula-7

Hakuwa na kazi ngumu kwenye mchezo wa jana kwani, Uganda hawakuwa na madhara makubwa pindi walipokuwa langoni mwa Stars.

Hata hivyo, alifanya kazi ya ziada mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kuokoa shuti la mbali la Moses Wasswa ambalo lilionekana kama lingekuwa bao.

Hassan Kessy-6

Alikosa utulivu katika dakika za mwanzoni za mchezo akifanya makosa kadhaa ambayo yangeweza kuipatia Uganda bao, lakini baadaye alitulia na kutimiza vyema majukumu yake.

Licha ya mwanzoni kuonekana kwenye hatari ya kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya njano dakika za mapema, alicheza vyema kiujumla.

Gadiel Michael-7

Alitengeneza muunganiko mzuri upande wa kushoto sambamba na Farid Mussa jambo lililovunja nguvu ya Uganda upande wa kulia.

Alitimiza vyema jukumu la kulinda na alipanda mara kwa mara kusaidia mashambulizi kwa kupiga krosi nzuri ambazo hata hivyo, ziliokolewa na mabeki wa Uganda.

Kelvin Yondani-7

Alimdhibiti vilivyo mshambuliaji Patrick Kaddu hasa kwenye mipira ya juu ambayo imekuwa ikitumiwa vyema na nyota huyo wa Uganda katika kufunga mabao yake.

Alijitahidi kucheza kwa nidhamu kubwa na baada ya Stars kupata mabao matatu hakutaka kuona mpira ukizagaa langoni mwake.

Aggrey Morris-8

Alikuwa imara katika kukabiliana na Farouk Miya, ambaye kabla ya mchezo ndiye alionekana ni miongoni mwa nyota hatari zaidi katika kikosi cha Uganda.

Juhudi zake binafsi zilimuwezesha kuifungia Stars bao la tatu baada ya kupiga kichwa kilichojaa wavuni akiunganisha krosi ya John Bocco, lakini ni yeye Morris aliyeanzisha shambulizi hilo kwa kumpasia mpira Bocco kutokana na mpira wa faulo.

Erasto Nyoni-8

Aliituliza vyema timu na kuziba mianya kwa viungo wa Uganda kupenyeza mipira. Aliwachezesha vizuri wenzake kutokana na pasi zake ambazo zilifika kwa usahihi.

Alifunga kwa ustadi mkwaju wa penati uliozaa bao la pili kwa Stars ambalo lilishusha presha ya umati wa mashabiki uliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa.

John Bocco-8

Amezoeleka kucheza kama mshambuliaji wa kati, lakini jana alipangwa kama winga wa kulia nafasi ambayo aliitendea haki vilivyo na kumlazimisha beki wa kushoto wa Uganda, Godfrey Walusimbi kutopanda mbele.

Nguvu na uwezo wake wa kumiliki mpira vilimfanya awe tishio kwa safu ya ulinzi ya Uganda. Alipiga krosi nyingi kuelekea langoni mwa Uganda na ndiye aliyepiga pasi iliyozaa bao la kuongoza la Stars, lakini pia ndiye alipiga krosi iliyounganishwa kwa kichwa na Morris na kuandika bao la tatu.

Mudathir Yahya-6

Alijitahidi kuunganisha na kuichezesha timu huku akishuka mara kwa mara chini kusaidiana na Erasto Nyoni katika kuilinda safu ya ulinzi ya Stars.

Hata hivyo kuna nyakati alionekana kukosa umakini na kupoteza pasi jambo ambalo liliiweka matatani Stars ingawa wachezaji wenzake walijitahidi kumfichia udhaifu wake.

Mbwana Samatta-8

Alionyesha ustaa wake kwa namna alivyokuwa anaufungua ukuta wa Uganda kwa chenga na uamuzi wake haraka pindi alipokuwa na mpira, ambapo pale alipotakiwa kupiga pasi alifanya hivyo pasipo kuchelewa lakini pale palipokuwa na ulazima wa kukokota hakusita kufanya hivyo na kwa usahihi mkubwa.

Alionekana ndiye mchezaji aliyeogopwa zaidi na ukuta wa Uganda uliiongozwa na kipa Dennis Onyango. Na ndiye alisababisha penalti iliyozaa bao la pili la Stars.

Saimon Msuva-9

Kasi yake ilionekana kuwapa tabu mabeki wa kati wa Uganda ambao maumbo yao makubwa yalionekana kuwafanya wacheze taratibu.

Alikuwa mwepesi wa kuingia kwenye eneo la hatari la Uganda na kufanya maamuzi na hilo lilizaa matunda katika dakika ya 20 alipoinasa pasi ya Bocco na kufanya uamuzi wa haraka wa kupiga shuti lililozaa bao la kuongoza.

Farid Mussa-7

Pengine kuanzishwa kwake kuliwashangaza wengi kwani, kwa muda mrefu amekuwa hapati nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza cha Stars.

Hata hivyo, hakuliangusha benchi la ufundi lililomuamini alifanya kazi kubwa na nzuri iliyozaa matunda. Kwanza alishuka kwa haraka kumsaidia beki wake Gadiel Michael, lakini pindi Stars ilipokuwa na mpira alikaa kwenye nafasi sahihi na kufanya maamuzi ya haraka yaliyowasumbua Uganda.

Pasi zake zilifikia walengwa kwa usahihi na kasi pamoja na uwezo wake wa kumiliki mpira, kukokota na kupiga chenga vilimfanya Nico Wadada kutopanda.

Walioingia

Himid Mao-5

Aliingia kuchukua nafasi ya Farid Musa na alitimiza vyema majukumu yake ambayo yalikuwa ni kuifanya timu iwe imara kwenye safu ya kiungo.

Feisal Salum-6

Alichukua nafasi ya John Bocco na ingawa muda ulikuwa umeshaenda, aliituliza timu kwa kupiga pasi na kumiliki mpira jambo lililopunguza presha ya Uganda iliyoonekana kuwa tishio dakika za mwisho.

Thomas Ulimwengu-3

Kuingia kwake kulilenga kupoteza muda ingawa hakuna kikubwa ambacho alikifanya kutokana na muda mdogo aliocheza.



Chanzo: mwananchi.co.tz