Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SportPesa Super Cup bado ngumu kwa klabu za Tanzania

39972 Pic+spotpesa SportPesa Super Cup bado ngumu kwa klabu za Tanzania

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa mwaka wa tatu mfululizo, klabu za Tanzania zimechemka kwenye mashindano ya SportPesa Super Cup tangu kuanzishwa kwake.

Mashindano hayo yamefanyika Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na Gor Mahia kutwaa ubingwa kwa kuilaza AFC Leopards mabao 3-0 katika mechi ya fainali.

Mwaka jana, mashindano hayo yalifanyika kule Kakamega nchini Kenya kwa Gor Mahia kuilaza Simba kwa mabao 2-0 na kutetea ubingwa wake kwa mwaka wa pili mfululizo.

Mashindano hayo yanayochezwa Kenya na Tanzania, mwaka huu yalifanyika Tanzania, lakini fainali ilichezwa na Kariobangi Sharks na Bandari. Sharks ilitwaa ubingwa kwa kuichapa Bandari bao 1-0.

Bandari ilikuwa ikishiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo, sawa na Mbao FC.

UBORA WA MASHINDANO

Timu za Kenya zilizoingia kwenye mashindano ya mwaka huu na pengine miaka mingine, zimeonyesha ubora wa hali ya juu. Timu za Tanzania zimekuwa zikihangaika kupata matokeo miaka yote.

Mabingwa, Kariobangi Sharks, Bandari FC, Gor Mahia na AFC Leopards zilionyesha umahiri kiasi cha kuzipa tabu timu za Tanzania.

Ingawa zilitolewa mapema, AFC Leopards na Gor zilicheza soka la kushambulia muda wote wa mchezo, zikiufungua uwanja kwa kupiga pasi ambazo ziliziweka kwenye wakati mgumu timu za Simba na Mbao ndani ya uwanja ingawa wapinzani wao waliibuka na ushindi.

Kwa upande wa Kariobangi Sharks na Bandari FC ambazo zilitinga hatua ya fainali, zenyewe zilicheza soka la kiufundi na nidhamu ya hali ya juu kimbinu ambalo lilizifanya timu pinzani kupata wakati mgumu wa kutawala na kumiliki mpira.

Katika mashindano hayo, ambacho kilizibeba timu za Kenya ni ubora na juhudi za mchezaji mmojammoja kwani walionyesha bidii ya kutaka kupata matokeo. Haikujaisha aina ya zawadi zaidi ya kupata heshima.

Kulikuwa na utofauti mkubwa baina yao na wachezaji wa timu za Tanzania. Nyota wengi wa timu za Kenya walionekana kucheza kwa hamasa, ari, kujitolea na nidhamu ya hali ya juu.

Kuonyesha kuwa hawakuwa na utani, tuzo mbili zilikwenda Kenya ambazo ni ile ya Mchezaji Bora na Mfungaji Bora. Tanzania iliambulia nafasi ya kipa bora wa mashindano.

Bingwa wa mashindano hayo atapambana na Everton wakati wa preseason ya Ligi Kuu ya England katika tarehe itakayopangwa. Marekebisho ya mwaka huu, bingwa akipatikana upande wa pili, mechi ya Everton itafanyika kwa timu bingwa.

Kimsingi mashindano hayo ya SportPesa yamekuwa yakiimarika na kujijengea jina siku hadi siku na kwa waliofuatilia mashindano ya mwaka huu watakiri kwamba yamekuwa na mvuto na msisimko wa hali ya juu kulinganisha na awamu zilizopita.

Simba, Yanga ziliharibu

Simba na Yanga hazikuwa na maajabu kabisa mwaka huu wa tatu mfululizo, timu hizo zimekuwa zikishiriki mashindano lakini bila ya ubingwa huku wakiziacha timu za Kenya kutamba.

Miamba hiyo ya Tanzania imekuwa ikiyatumia mashindano hayo ya SportPesa kama sehemu ya mazoezi yao ya kujiandaa na mashindano mengine na pia kujaribu baadhi ya wachezaji ambao zinalenga kuwasajili.

Kitendo cha kufanya vibaya kwenye mashindano hayo, kunazinyima fursa muhimu timu hizo ikiwemo kukosa kucheza na Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Kucheza na Everton ni nafasi kwa wachezaji kujitangaza na kujiuza, ni fursa muhimu ya kubeba sekta ya utalii hapa nchini lakini pia kungezipatia timu hizo fedha ambazo zingesaidia uendeshaji wa klabu kwenye baadhi ya mambo.

Ligi ya Kenya yachomoza

Kufanya vizuri kwa timu za Kenya ni wazi inaonyesha wana ligi makini. Tangu mashindano hayo yaanzishwe, ni timu moja tu ya Tanzania iliyowahi kufika fainali ambayo ni Simba lakini hata hivyo ilipoteza mbele ya Gor Mahia mwaka 2018 kwa kufungwa mabao 2-0.

Kitendo cha timu za Kenya kutawala kwenye mashindano hayo na kiwango kibovu kinachoonyeshwa na timu za hapa nchini, kinajenga taswira isiyo nzuri kwa ligi yetu na pengine kinatoa ishara kuwa bado ligi yetu sio imara.

Mbao FC ilijitutumua

Hakuna namna unayoweza kuwasifu kwa kuutendea haki mwaliko wa michuano hiyo kwa kuwa hawana udhamini wa SportPesa.

Mbao FC ambayo ni zaidi ya ‘Kiboko ya Vigogo’ wamekuwa mwiba kwa Simba na Yanga pindi wanapokutana nazo kwenye mechi zinazochezwa jijini Mwanza.

Mwaka huu walialikwa kushiriki mashindano ya SportPesa na walishtua wengi baada ya kuwatupa nje mabingwa watetezi, Gor Mahia kwa mikwaju ya penati 4-3.

Pamoja na kutofanikiwa kutinga hatua ya fainali, Mbao walicheza kwa nidhamu kubwa kwenye mashindano hayo na ndio maana haikushangaza kuona mechi zao dhidi ya timu ngumu na nzuri za Gor Mahia na Kariobangi Sharks ziliishia kwenye mikwaju ya penati baada ya kutoka sare ya dakika 90.

Kagame Cup inaanza kuzikwa

Kadri muda unavyozidi kwenda, mashindano ya SportPesa yanazidi kuyaweka kwenye wakati mgumu yale ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup).

Mpangilio wa mashindano ya SportPesa umekuwa ni mzuri na wamekuwa wakitoa huduma stahiki kwa timu huku wakifanikiwa kuyapa msukumo mkubwa licha ya kushirikisha nchi chache tofauti na yale ya Kagame ambayo yamekuwa yakifanyika kwa kusuasua.

Uzoefu umembeba Mwalala

Singida United na Simba zote zilifia mikononi mwa Bandari FC ya Kenya inayofundishwa na nyota wa zamani wa Yanga, Ben Mwalala.

Inavyoonekana Mwalala ametumia vyema uzoefu alionao kwa soka la Tanzania ambalo amelitumikia kwa muda mrefu, kuzimaliza Simba na Singida United.

Waliobamba

Kundi kubwa la nyota walioshiriki mashindano hayo mwaka huu limefanikiwa kuonyesha kiwango kizuri ambacho kimekuwa na msisimko kwa mashabiki.

Hata hivyo, wachezaji kama Ibrahim Njoole na Rafael Siame (Mbao FC),Mwendwa Harrison, Duke Abuya na George Abege (Kariobangi Sharks) na Hamisi Abdallah pamoja na William Wadri (Bandari FC) walikuwa moto wa kuotea mbali.



Chanzo: mwananchi.co.tz