Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri yafichuka kipigo Stars

27939 Pic+siri TanzaniaWeb

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maseru/Dar Hakuna sababu ya msingi ambayo Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, anaweza kuitoa kama utetezi baada ya kipigo cha bao 1-0 ilichopata timu hiyo ugenini dhidi ya Lesotho, juzi.

Mpasuko, hesabu, mbinu na maandalizi duni ya benchi la ufundi hapana shaka vilichangia timu ya Taifa kushindwa kuibuka na ushindi ambao ungeiwezesha kukaribia kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Cameroon, mwakani.

Kabla ya mchezo kuanza kulikuwa na dalili ya wazi kuwa Taifa Stars ingepoteza mechi hiyo kinyume na matarajio ya wengi kuwa ingeibuka na ushindi kutokana na hamasa ya nje ya uwanja iliyokuwepo kwa wadau wa soka Tanzania.

Amunike na benchi lake la ufundi licha ya kupewa muda wa kutosha wa zaidi ya siku 10 kujiandaa kwa mchezo huo tena ikiweka kambi nchini Afrika Kusini, alipoteza ushawishi kwa wachezaji na kusababisha uwepo mpasuko ndani ya timu ambao ulifanywa siri kubwa kutokana na mazingira halisi ya mchezo husika.

Mpasuko na mgogoro huo wa ndani ya timu ulisababisha beki wa kimataifa wa Tanzania anayecheza Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda kutopangwa wala kuwekwa benchi kwenye mechi ya juzi licha ya uzoefu alionao na kiwango bora alichonacho kwa sasa.

Banda ambaye ni beki tegemeo na nahodha msaidizi wa Baroka, ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani, hivyo uwepo wake ungewezesha benchi la ufundi kuwa na wigo mpana wa kufanya mabadiliko kwa namna yoyote ile wakati mchezo ukiendelea.

Mbali na hilo, Amunike alijaza kundi kubwa la wachezaji ambao kiasili ni walinzi jambo lililosababisha timu icheze muda mrefu kwa kujilinda huku safu ya ushambuliaji ikiundwa na washambuliaji wawili walioanza kwenye kikosi cha kwanza, Saimon Msuva na Shabani Idd waliokosa huduma sahihi uwanjani.

Kundi hilo liliundwa na Gadiel Michael, Ally Abdulkarim, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Abdallah Kheri, Himid Mao na Mudathir Yahya.

Baada ya Taifa Stars kufanya mabadiliko kipindi pili kuwatoa Gadiel, Kheri, Mudathir na nafasi zao kuchukuliwa na Shiza Kichuya, John Bocco na Feisal Salum, ilipata uhai kwa kutawala mchezo na kushambulia mara kwa mara ingawa muda ulibaki mfupi kabla ya mpira kumalizika.

Katika hali ya kushangaza Kheri aliyecheza beki wa kulia, huwa hachezi kwenye nafasi hiyo na kiasili ni beki wa kati na upande aliokuwa akicheza ndio ulionekana kuwa dhaifu.

Kitendo cha Amunike kulazimisha kumpanga beki huyo upande wa kulia, kilizua maswali zaidi kwa kuwa katika benchi walikuwepo mabeki wawili wanaocheza upande wa kulia.

Mabeki hao ni Hassani Kessy ambaye hivi karibuni ameiongoza Nkana Red Devils kutwaa Kombe la Chama cha Soka Zambia na Salum Kimenya ambaye amekuwa nyota muhimu kwenye kikosi cha Prisons kutokana na uwezo wake wa kuzalisha na kufunga mabao.

Amunike amejitetea akidai wachezaji walishindwa kufuata alichowaelekeza na kufungwa hakukutokana na mbinu zake kushindwa kufanya kazi.

“Nadhani kiujumla timu nzima haikucheza vizuri na hatukuwa na nidhamu kwa kufanya makosa mengi ya mchezaji mmoja mmoja ambayo yametugharimu.

“Niliwaonya mapema wachezaji wangu na kuwaambia ugumu wa hili kundi, lakini mwisho hatukuweza kuwa na ule ubora ambao tuliutegemea,” alisema Amunike.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe alisema Watanzania wanatakiwa kushikamana na kutopoteza matumaini baada ya kupoteza mchezo huo.

“Mimi naamini bado nafasi tunayo hatupaswi kuanza kunyoosheana vidole na kumtupia mtu fulani lawama, badala yake tunapaswa kuwa kitu kimoja ili tuweze kushinda mchezo wa mwisho na kupata nafasi ya kwenda Cameroon,” alisema Dk Mwakyembe.

Kwa nyakati tofauti, makocha na wachambuzi wa soka wamempa mbinu Amunike ya kujiweka salama katika mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda Machi 24, mwakani.

Pia miongoni mwao wamemkingia kifua Amunike wakidai kocha ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kupanga kikosi kulingana na mahitaji ya mechi husika.

“Tatizo tumekariri lazima mchezaji fulani acheze, asipocheza ndiyo tunakosoa kikosi cha kocha, binafsi sikubaliani na wanaopinga timu ya kocha, ila mfumo wa kujihami aliotumia ulifeli. Kuna njia mbili za kujihami, kurudi nyuma kama ilivyotokea jana (juzi) au kushambulia ili wapinzani wasije langoni mwako.

“Kwa mechi ya jana (juzi) ulinzi ilikuwa lazima, lakini pia tulipaswa kushambulia zaidi hata katika mechi ya mwisho na Uganda benchi la ufundi liangalie kitu kama hicho.

“Tuna mechi ya mwisho nyumbani tufanye tuwezavyo tusiwatoe wachezaji mchezoni, pia wachezaji wajitambue watambue jukumu la kufuzu liko mikononi mwao, lakini kwa kipindi hiki, kocha apewe muda wa kuwa na wachezaji wake angalau siku mbili kwa mwezi kuanzia sasa na itakapofika Februari apewe fursa ya kukutana na wachezaji japo kwa wiki mara moja ili kuendelea kutengeneza mfumo wake,” alisema Msolla.

Mchambuzi Ally Mayay alisema Amunike alipaswa kuendelea na kikosi kilichocheza mechi ya marudiano dhidi ya Cape Verde na angeziba nafasi chache za wachezaji waliocheza mechi hiyo.

“Sijui sababu ya kocha kuweka walinzi wengi jana (juzi), plani ya kocha ilifeli, sisi kufungwa na Lesotho hakumaanishi wale ni wazuri sana lakini walionekana bora kutokana na sisi kukosea ‘game plan,” alisema Mayay.

Alisema katika maandalizi na mechi na Uganda, Amunike aweke utaratibu wa kufuatilia viwango vya wachezaji akitumia mbinu za makocha wa timu za Taifa za Ulaya kwa kuwa nafasi ya kufuzu bado ipo.

Kocha na mchezaji wa zamani wa Taifa Stars iliyofuzu Afcon mwaka 1980, Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Amunike alikuwa sahihi kupanga kikosi hicho, lakini tatizo wachezaji wengine hawajui mpira.

“Amunike amekuja kufanya kazi, sio kuharibu, hivyo timu aliyoipanga ilimshawishi katika mazoezi, lakini wakashindwa kufanya kile kocha alichokitarajia kwenye mechi,” alisema Rishard.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema ni wajibu wa wachezaji kujitoa kwa uwezo wao wote ili kupata nafasi hiyo kwa kuhakikisha wanashinda dhidi ya Uganda.



Chanzo: mwananchi.co.tz