Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siri Yanga, Azam FC kuitaka nafasi ya pili

Yanga11azam Siri Yanga, Azam FC kuitaka nafasi ya pili

Wed, 15 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKATI Klabu ya Yanga na Azam zikipigana vikumbo kuwania kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu msimu huu, Nipashe limebaini siri kubwa inazozifanya klabu hizo kutoana jasho kuisaka nafasi hiyo.

Tayari Simba imetwaa ubingwa wa ligi hiyo ambayo imebakiza mechi nne kabla ya kumalizika msimu huu, hivyo kujihakikishia nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, timu yenye tiketi hiyo nchini, ni Namungo FC ambayo imetinga fainali ya Kombe la FA na sasa itakutana na Simba Agosti 2, mwaka huu katika Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, hivyo hata kama Wekundu wa Msimbazi wakishinda uwakilishi huo utabaki kwa Namungo kwa kuwa yenyewe itaiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa.

Hata hivyo, wakati akizungumza na mwandishi wetu jana kuelekea mchezo wao wa leo utakaopigwa katika Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar, Kocha Mkuu wa Azam FC, Mromania Aristica Cioaba, alisema malengo yake ni kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ili kama Tanzania itapata tena nafasi nne za kushiriki mashindano ya kimataifa bahati hiyo iwaangukie.

Alisema mipango yao imevurugika kutokana na kutolewa kwenye michuano ya FA Cup, lakini watahakikisha sasa wanamaliza wa pili ili kuvizia nafasi hiyo endapo itajitokeza tena kama msimu uliopita.

Azam FC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 65 baada ya mechi 34, ikiwa ni pointi moja mbele ya Yanga ambayo nayo itashuka katika Uwanja wa Taifa leo kuikaribisha Singida United inayoburuza mkia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live