Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Singida United, Eliuter Mpepo ametuma salamu kwa timu tatu za mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo Yanga.
Akizungumza kwa simu jana, Mpepo alisema mkakati ni kupata pointi tisa katika mechi tatu ambazo Singida United itakuwa jijini kabla ya kurejea mkoani Singida.
Mpepo alidai pointi tisa zitaiweka Singida United katika mazingira bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuingia katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu.
Singida United itakuwa na kibarua kigumu leo itakapovaana na African Lyon ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC.
Mchezaji huyo wa zamani wa Tanzania Prisons ya Mbeya, alisema baada ya kumalizana na African Lyon, wataigeukia Yanga katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa Septemba 23.
“Mwanzo mzuri wa ligi utarahisisha kazi mwishoni, tumepanga kushinda katika kila mchezo na mkakati wetu ni kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
Baada ya kucheza michezo mitatu Dar es Salaam, Singida United itarejea Singida ambapo itaikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Namfua, Septemba 26.
Singida United iliyopoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Biashara United ilipofungwa bao 1-0, ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Wakati huo huo, Kocha msaidizi wa African Lyon, Adam Kipatacho alisema wataendelea kutumia mfumo mpya 4-4-2 ambao unatoa fursa kwa timu kucheza kwa kushambulia na kukaba haraka.