Dar es Salaam. Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki (Cecafa) limethibitisha nafasi za Yanga kuwa itachukuliwa na Singida United kwenye Kombe la Kagame ambalo litaanza kutimua vumbi nchini Juni 29, hadi Julai 13.
Yanga ilitangaza kujitoa kwenye michuano hiyo maarufu ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa lengo la kupumzisha kikosi chao kabla ya kuendelea na michezo ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika, Julai 18 ambapo wao watakipiga na Gor Mahia ya Kenya ugenini.
Mbali na Yanga klabu ya St. George ya nchini Ethiopia pia walijitoa na baraza hilo likaipa nafasi klabu ya APR ya Rwanda ili kuziba nafasi yao.
Klabu zitakazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na Simba, Azam FC pamoja na Singida United za Tanzania Bara, JKU ya Zanzibar na Rayon Sports ya Rwanda.
Nyingine ni Dakadaka ya Somalia, Ports ya Djibouti, Lydia Ludic ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya, St. George ya Ethiopia, Kator FC ya Sudan Kusini na Vipers SC ya Uganda.
Cecafa pia imethibitisha Kombe la Chalenji kwa wanawake litafanyika nchini Rwanda kuanzia Julai 19 hadi 29 mwaka huu.
Mataifa yanayo tarajiwa kushiriki ni Rwanda, Kenya, Uganda, Tanzania, Djibouti, Zanzibar na Ethiopia.