Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Sinema’ ya kina Malinzi walivyoondoka gerezani

88345 Pic+malinzi ‘Sinema’ ya kina Malinzi walivyoondoka gerezani

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ilikuwa ni kama sinema vile, pale rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi alipokuwa akitoka gerezani Keko jijini Dar es Salaam jana, baada ya kufanikiwa kulipa faini ya Sh500,000 aliyotozwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, juzi.

Jana asubuhi, wakiwa na nyuso za matumaini ndugu, jamaa na marafiki wachache wa Malinzi na aliyekuwa katibu mkuu wa TFF enzi za utawala wake, Celestine Mwesigwa, walitumia saa 2:14 kukamilisha taratibu gerezani hapo na kurejea uraiani na viongozi hao wa zamani wa mpira waliokaa rumande kwenye gereza la mahabusu Keko kwa siku 897.

Malinzi na Mwesigwa walitoka gerezani saa 5.14 asubuhi baada ya mahakama hiyo kuwahukumu kwenda jela au kulipa faini juzi. Baada ya hukumu hiyo walirejeshwa gerezani Keko kabla ya jana ndugu zao kulipa faini na kuwasilisha risiti za malipo hayo gerezani na kuachiwa huru.

Hali ilivyokuwa

Ndugu, jamaa na marafiki wasiozidi wanane waliwasili gerezani hapo saa 3.00 asubuhi wakiwa na risiti ya malipo ya faini wakiongozwa na mwanasheria wao, Lucy Ngongoseke na mmoja wa ndugu wa Malinzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Julius huku wengine watano wakisubiri nje ya uzio wa gereza.

Saa 5.00 gari dogo aina ya Mark II nyeupe liliruhusiwa kupita kwenye geti la gereza na dakika 14 baadaye likatoka likiwa limewabeba Malinzi na Mwesigwa huku gari nyingine mbili, IST nyekundu na Toyota Wish nyeusi zilizowabeba ndugu, jamaa na marafiki zikifuata nyuma kutoka eneo la gereza.

Awali ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa eneo hilo walipanga msafara uanzie kanisani kabla ya kwenda nyumbani.

“Kwa kuwa Mungu ndiye ameamua hili lililofanyika leo litokee, hatuna budi kwenda kanisani kumshukuru kabla ya kwenda nyumbani,” alisema Ngongoseke.

Hata hivyo, msafara huo ulipishana ambapo dereva wa gari aina ya Wish alikwenda hadi kanisa la St Joseph lililopo Posta na kuzunguka eneo la kanisa kabla ya kutoka saa 05.48 na kuelekea kanisa la St Peters, Oysterbay, ambako pia lilizunguka na kutoka, kisha kuelekea nyumbani alikokuwa akiishi Malinzi, Mikocheni.

Katika nyumba hiyo ambayo sasa ni hoteli, gari nyeupe aina ya Mark II ilikuwa ndani ya uzio na Toyota Wish nyeusi iliyokuwa kwenye msafara wakati wakitoka gerezani ikiwa imeegeshwa nje ya nyumba hiyo.

“Baadhi ya watu waliojitokeza gerezani kuwachukua Malinzi na Mwesigwa walipishana, wengine wakiingia na kutoka kwenye nyumba hiyo ambapo hata hivyo hawakuruhusu mtu mwingine tofauti na wao kuingia ndani,” alisema mmoja wawatu wao wa karibu.

“Hatuhitaji mtu kwa sasa, isitoshe Malinzi hayuko hapa na hata kama angekuwepo haturuhusu mtu mwingine tofauti na familia kuonana naye.”

Majirani wa eneo la nyumba hiyo walikuwa wamekaa vikundi kwenye maduka mawili yaliyopo sehemu hiyo baadhi yao wakijadili kuachiwa kwa rais huyo wa zamani wa TFF. Malinzi na Mwesigwa wamekwepa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukubali kulipa faini ya Sh500,000 kwa Malinzi ambaye alipatikana na kosa la kughushi nyaraka.

Mwesigwa kwa upande wake alitakiwa kulipa faini ya Sh1,000,000 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kutengeneza nyaraka ya uongo na kuitumia.

Malinzi na Mwesigwa walikamatwa Juni 27, 2017 na kupandishwa kizimbani mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 29 pamoja na aliyekuwa mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, wakikabiliwa na mashtaka 28 ikiwamo kughushi na utakatishaji wa Dola za Marekani 375,418.

Chanzo: mwananchi.co.tz