Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simbu ajilipua Olimpiki 2024

Simbu Olimpiki Simbu ajilipua Olimpiki 2024

Sat, 20 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nahodha wa Tanzania katika Michezo ya Olimpiki, Alphonce Simbu ni kama amejilipua kwa kuahidi kwamba safari hii ataingia kwenye tatu bora ya michezo hiyo inayofanyikia Paris Ufaransa.

Simbu ataiongoza timu ya Tanzania kwenye michezo ya msimu huu itakayofunguliwa Julai 26 hadi Agosti 11 jijinj Paris Ufaransa.

Wengine watakaoiwakilisha nchi waogeleaji Collins Saliboko na Sophia Latiff, mcheza judo, Andrew Mlugu na wanariadha, Jackline Sakilu, Magdalena Shauri, Simbu na Gabriel Geay.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Julai 19,2024 Simbu amesema licha ya mbio ya marathoni kuwashindanisha magwiji wa dunia akiwamo Kenenisa Bekele wa Ethiopia, haitawakwamisha kufanya vizuri.

"Huu ni mwaka wetu, maandalizi tuliyofanya hakuna shaka kwenye top three (tatu bora) ya marathoni msimu huu Tanzania itakuwa ni miongoni.

Simbu na Geay kwa mara ya kwanza watashiriki mbio moja, jambo ambalo Simbu anasema linawaongezea morali ya kupambana na kuhamasishana kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa wanariadha wa nchi nyingine hasa Kenya na Ethiopia.

Mbali na nyota hao, msafara wa Tanzania pia kwenye michezo hiyo itakuwa na makocha, Anthony Mwingereza (riadha), Alex Mwaipasi (kuogelea) na Innocent Mallya (judo) watakaombatana na mkuu wa msafara, Henry Tandau, mwandishi wa habari, Muhidin Michuzi na daktari wa timu, Eliasa Mkongo.

Akikabidhi bendera ya taifa kwa timu hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Suleiman Serera amesema nchi ina waamini wanamichezo hao kwamba hawataweza kuwaangusha.

"Rais (Samia Suluhu Hassan) ametutuma tuwaeleze kuwa atafuatilia mashindano yenu, nchi iko pamoja na ninyi na Serikali itawagharamia posho zenu ili mwende Paris bila mawazo," amesema.

Amesema, mwisho wa mashindano ya msimu huu ndio utakuwa mwanzo wa maandalizi ya michezo ya 2028, akisisitiza mipango lazima ipangwe mapema.

"Nakuagiza Katibu mtendaji wa BMT (Baraza la Michezo la Taifa) mkae na vyama tujipange ili twende mbele na kupata wachezaji wengi zaidi," amesema.

Amesema nchi ipo kwenye kipindi cha neema hivi sasa na wanamichezo wasipoutumia wakati huu hawafahamu huko mbele itakuwaje?.

"Bajeti ya michezo imeongezeka mara dufu, huko nyuma tulikuwa tunapewa zaidi ya Sh 30bilioni, lakini sasa ni Sh 285bilioni ambazo ukiachana na matumizi ya kawaida, vyama na mashirikisho ya michezo nchini yaangalie pesa hizo yatazifanyia nini?.

Hata hivyo, Serera amewashauri wanamichezo kujitunza akimtolea mfano Simbu ambaye alisema mwaka 2015 yeye Serera akiwa masomoni, Beijing China mwanariadha huyo alikuwa anatamba na hadi sasa bado anafanya vizuri.

Mchezaji mwenyewe unatakiwa ujitubze, nikiwa Beijing basoma mpokea Simbu, hadi leo ipo

Awali, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema msafara wa Tanzania kwenye michezo hiyo utaondoka nchini kwa mafungu.

Kundi la kwanza litaondoka Julai 22 likiwa na mkuu wa msafara, Henry Tandau, kundi la pili litaondoka Julai 23 na kundi la mwisho ni la wanariadha litakaloondoka Agosti 7 tayari kwa michezo hiyo itakayofunguliwa Julai 26 hadi Agosti 11.

Alisema, maandalizi ya TOC yalianza Januari 2022 kwa wanamichezo watano kupata udhamini wa Kitengo cha misaada cha Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (Olympic solidarity) ambao ni Simbu, Geay, Failuna Abdi, Mlugu na muogeleaji, Hilal Hilal.

"Kati yao, Simbu na Geay walifikia viwango, Mlugu alipata nafasi ya upendeleo kushiriki Olimpiki na Hilal na Failuna hawakufuzu," alisema.

Alisema kwenye kuogekea, Collins ambaye alipata udhamini wa shirikisho la kimataifa la mchezo huo pia alipata nafasi ya upendeleo na Sophia huku kwa bondia, Yusuph Changalawe ambaye TOC na BMT zilimsapoti kushiriki mashindano ya kufuzu mara tatu alishindwa kufuzu na walipomuombea nafasi ya upendeleo pia alikosa.

Katika maandalizi hayo, Bayi alisema TOC imekwishatumia zaidi ya Sh 406milioni.

Mkuu wa masafara wa Tanzania kwenye michezo hiyo, Henry Tandau alisema safari ya timu imekamilika na kwenye ufunguzi bendera ya Tanzania itabebwa na Sophia na Mlugu.

"Nahodha (Simbu) kwenye ufunguzi atakuwa hajawasili Paris.

Viongozi wengine watakaokuwa kwenye msafara huo ni

Waziri wa michezo, Damas Ndumbaro na msaidizi wake, rais wa TOC, Gulam Rashid na Bayi watakaokwenda kwa ajili ya vikao.

Awali, harakati za kufuzu zilishirikisha pia timu ya soka la wanawake, ngumi na brake dance ambazo zilishindwa kufikia viwango huku Tanzania ikishiriki michezo hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kutwaa medali mbili za fedha kwenye Olimpiki ya 1980 huko Moscow, Russia.

Chanzo: Mwanaspoti