Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yazidi kuchanja mbuga

Af5063e4036d9cb4a5963b01dbd46912 Simba yazidi kuchanja mbuga

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SIMBA Queens imeendelea kulikaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu soka la Wanawake Tanzania Bara baada ya kuifunga Kigoma Sisters kwa mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma juzi.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 44 baada ya kucheza michezo 17 ikifuatiwa na JKT Queens ambayo ina pointi 39 baada juzi kuifunga Panama katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam. Katika mchezo huo mabao ya Simba Queens mawili yalifungwa na Oppah Clement na Mwanahamisi Omar na lile la Kigoma Sisterz lilifungwa na Aisha Hamza na Kigoma kuendelea kubaki na pointi zake 23.

JKT Queens ikicheza Uwanja wa Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam iliifunga Panama Queens ya Iringa kwa mabao 8-0, na mabao matano yaliwekwa kimiana na Stumai Abdallah na matatu yalifungwa na Fatuma Mustapha.

Nayo Yanga Princess ikicheza kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam iliifunga Ruvuma Queens kwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Amina Bilal na kufikisha pointi 29 katika nafasi ya tano huku Ruvuma Queens ikendelea kubaki na pointi zake 35.

Ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Amri Abeid Arusha, Tanzanite iliifunga TSC ya Mwanza kwa mabao 3-0 na mabao hayo yalifungwa na Mariam Dickson, Asnath Linus na Esther Massawe na kufikisha pointi 13.

Alliance Girls ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, iliwafunga wenyeji Baobab kwa 1-0 bao pekee la Aisha Khamis na kufikisha pointi 37 katika nafasi ya tatu na Baobab wanabaki na pointi zao 19.

Katika Uwanja wa Nyamagana Mwanza, Mlandizi Queens iliifunga Marsh kwa mabao 3-1 na kufikisha pointi 26, mabao ya Mlandizi yalifungwa na Sheha Mohamed, Philomena Daniel na Herieth Kulwa wa Marsh alijifunga na Rose Mpoma akafunga bao moja.

Katika orodha ya wafungaji, Fatuma Mustapha wa JKT Queens anaongoza kwa kufunga mabao 26 akifuatiwa na Asha Rashid wa JKT Queens mwenye mabao 19, Asha Hamza wa Kigoma Sisterz ana mabao 15.

Stumai Abdallah ana mabao 14, Mwanahamisi Omari wa Simba Queens ana mabao 13, Asha Djafar na Oppah Clement wa Simba wana mabao 12, Amina Ramadhani wa Ruvuma, Aisha Juma wa Alliance na Amina Ramadhan wa Ruvuma kila mmoja ana mabao 10.

Chanzo: habarileo.co.tz