Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yatia mkono usajili Yanga

89227 Simba+pic Simba yatia mkono usajili Yanga

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

HUKO mtaani kwa sasa stori kubwa ni ishu za usajili unaoendelea nchini kupitia dirisha dogo lililofunguliwa Jumatatu, ambapo Yanga imeonekana imekuja kivingine kwa kufanya usajili kwa fujo na leo Jumatano mashabiki wake wanaanza kuhesabu saa kabla ya kumpokea winga mpya.

Luis Jose Miquissone inaelezwa yupo njiani kuja kumalizana na Yanga, lakini taarifa mbaya ni kwamba mabosi wa Msimbazi ghafla wameamua kutia mkono kwenye usajili huo wa Jangwani.

Habari ambazo Mwanaspoti imezinasa ni kwamba, mabosi wa Simba wamejitosa jumla kuwania saini ya winga huyo aliyewatibulia kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika alipokuja nchini na UD Songo ya Msumbiji.

Inaelezwa, winga huyo matata ameshatumiwa tiketi pamoja na nakala ya mkataba ili aupitie kupitia wakala wake kutoka Kampuni ya Wimbi Foot, lakini fasta Simba walipozinasa taarifa hizo nao wakaona isiwe tabu na kumtwangia simu wakitaka kumpa dau nono ili atue Msimbazi.

Kumbuka awali Mwanaspoti liliripoti, Simba walikuwa wakimpigia hesabu Miquissone ili kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi, lakini wakampotezea na matajiri wa Yanga wakaamua kumtwangia simu akiwa kwao na kufanya mazungumzo na Mwanaspoti liliripoti dili zima la winga huyo.

Timu zote, zilimuona Miquissone aliyekuwa pia nahodha wa UD Songo, wakati alipoupiga mpira mwingi kwenye mechi zote mbili dhidi ya Simba, na katika mchezo wa marudiano jijini Dar ndiye aliyefunga bao lililoing’oa Simba hatua ya awali kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya 1-1.

Yanga kupitia wadhamini wao Kampuni ya GMS, wanadaiwa wamemtumia tiketi mchezaji huyo ili aje nchini akiwa na wakala wake baada ya kuzungumza na kukubaliana masuala ya kimkataba na kilichobaki ni kusaini.

Mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga, aliliambia Mwanaspoti kuwa wamezungumza na mchezaji huyo pamoja na wakala wake ambao walikubaliana kumtumia tiketi ya ndege kuja nchini na kumsainisha mkataba wa miaka miwili kama ambavyo wamekubaliana.

“Tumemtumia tiketi ili aje nchini na mazungumzo hayatakuwa marefu kwani tulizungumza siku nyingi nyuma na kitakachokuwa mbele yetu ni kusainishana mkataba endapo mambo yatakuwa kama tulivyokubaliana,” alisema kiongozi huyo.

Lakini wakati mabosi wa Yanga wakimsubiri kwa hamu Miquissone, tayari Simba nao wameingiza mkono kwa kumtwangia simu wakimshawishi atue Msimbazi kwa dau zaidi ya lile aliloahidiwa na Yanga.

Taarifa za ndani kutoka Simba, zinadokeza, Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza amemtwangia simu na kuzungumza naye kuona jinsi gani wanaweza kumnasa licha ya kuwa tayari Yanga wamefanya mazungumzo naye kufikia hatua ya kumtumia tiketi ya ndege.

Mwanaspoti baada ya kupata taarifa hizo lilimsaka Senzo anayeelezwa anamfahamu winga huyo tangu akiwa timu ya Chippa United, inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ila hakupatikana hewani na hata ujumbe aliokuwa akitumiwa kwenye Whatsapp alikuwa akiusoma bila kujibu.

MSIKIE MWENYEWE

Miquissone alisema muda huu yupo likizo anaendelea na mapumziko yake baada ya kumaliza Ligi Kuu ya Msumbiji na mashindano mengine yote kwa maana hiyo masuala yake ya kwenda timu nyingine amemuachia wakala wake.

“Kwa sasa sitaki kuongea sana na vyombo vya habari, ila ni kweli Simba nimezungumza nao ila maongezi hayakuwa marefu tofauti na ilivyokuwa kwa Yanga walionyesha wapo siriazi na kutaka kunisajili,” alisema Miquissone.

“Uhakika wa Yanga unatokana na wao kuzungumza mpaka na wakala wangu waliyekubaliana kutumiana tiketi ya ndege ili nije Tanzania kuzungumza nao na kusaini mkataba, ila hata Simba nao mazungumzo yetu hayakuwa mabaya kwa maana hiyo lolote linaweza kutokea,” alisema.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, aliweka picha ya Miquissone, akimpigia chenga beki wa Simba, Gadiel Michael na kuandika maneno ya mafumbo akiwatambia watani wao wa jadi... ‘Asiyejua maana haambiwi maana lisemwalo....’

Posti hiyo inaonyesha Bumbuli anaamini kuwa mchezji huyo anatua kwenye kikosi cha timu yake.

Chanzo: mwananchi.co.tz