Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yataka viongozi Yanga wajitathmini

10199 Yanga+pic TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni kutokana na sintofahamu inayoendelea ndani ya klabu kwani hali hiyo inadhoofisha uimara wa timu.

Dar es salaam. Wakati Simba inawasili leo alfajiri kutoka nchini Uturuki ilikoweka kambi kwa wiki mbili, hasimu wao Yanga walikuwa wakijipanga kutua ‘Mji Kasoro’ kwa ajili ya maandalizi ya mechi za Ligi Kuu na mechi za Kimataifa.

Yanga inacheza Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa imesaliwa na mechi mbili za kukamilisha ratiba, dhidi ya USM Alger ya Algeria na ile ya Rayon Sport nchini Rwanda.

Yanga yenye pointi moja, ikishinda mechi zote, itafikisha pointi saba ambazo tayari zimevukwa na Gor Mahia na USM Alger.

Simba inayonolewa na Patrick Aussems akisaidiwa na Masoud Djuma ilipiga kambi kujiandaa na mechi za Ligi Kuu na zile za kimatiafa zinazoikabili timu hiyo.

Pamoja na hayo, hizo siyo hoja sana, hoja ni kwamba, Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Abdallah Salim ‘TryAgain’ amesema wanasononeshwa na hali ilivyo ndani ya klabu ya Yanga na kwamba wakati umefika wanaoongoza Yanga wanatakiwa wenyewe kujitathmini.

“Ukiniuliza ishu ya Yanga na hali yao, ni kweli tunaona wana matatizo, lakini wanakosea wapi, hapa ni viongozi wao tu,” alisema kiongozi huyo akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu.

“Ukiangalia sisi na Yanga tunapata fedha sawa, kama fedha za wadhamini SportPesa tunapata sawa, kama zile za Azam tunapata sawa, hapa kutakuwa na tatizo.

“Yanga kuna mahala viongozi wanakosea ndiyo sababu ya shida zote hizi zinazowakabili,” alisema TryAgain.

Hata hivyo, alisema anaamini wachezaji watajituma kwa kuwa ni kazi yao, licha ya kuwa itawawia vigumu kutuliza akili wakati klabuni hakujatulia.

“Hatuwezi kufurahia kinachoendelea Yanga, matatizo ya Yanga yanahitaji kutatuliwa kwa busara, maarifa na weledi wa hali ya juu pamoja na kuwajenga wachezaji kisaikolojia na zaidi ni viongozi kujitathmini,” alisema.

Alisema uimara wa Simba ya sasa unahitaji kuona Yanga na yenyewe inakuwa imara kwa maana ya kwamba wachezaji wanakuwa wametimia kila idara kwa pande zote ili kutoa ushindani.

“Simba imara lazima na Yanga iwe imara, hapa ndipo kuna ushindani, ni jukumu la mwalimu kuisuka timu pamoja na kuwajenga wachezaji kisaikolojia, lakini pia viongozi kujiangalia wamekosea wapi kwani Yanga ni kama sisi (Simba) hasa kwenye udhamini kwani udhamini wao na Simba haupishani tatizo ni nini sasa hapa?” alihoji TryAgain.

Miaka miwili iliyopita, Yanga ikiwa chini ya mwenyekiti wake, Yusuf Manji, iliwahi kwenda kupiga kambi nchini Uturuki pamoja na kufanya vizuri mechi zake za ligi na kutwaa ubingwa mara tatu.

Chanzo: mwananchi.co.tz