Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yataja wakusajiliwa

Kocha Simba.webp Kocha Mkuu wa Simba FC

Wed, 15 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wamo wa kimataifa wawili, straika na beki, huku pia ikimulika wengine kutoka...

BAADA ya kuwaadhibu watani zao, Yanga kwa kipigo cha mbwa mwizi kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka nchini maarufu FA Cup, mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba wametaja idara wanazotarajia kuziboresha katika kikosi chao kuelekea msimu ujao.

Mwishoni mwa wiki Simba ilipata ushindi wa mabao 4-1 kwenye mechi hiyo ya nusu fainali dhidi ya Yanga iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, hivyo sasa itakutana na Namungo FC iliyoitoa Sahare All-Stars kwa bao 1-0.

Mechi hiyo ya fainali ambayo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na ubora wa timu hizo mbili, itapigwa katika Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa Agosti 2, mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu mpango wa kukiboresha kikosi chao, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema wanatarajia kuongeza wachezaji wasiozidi wanne katika dirisha la usajili lijalo ili kukiimarisha kikosi chao kuelekea michuano ya kimataifa, Ligi Kuu na michuano mingine msimu ujao.

Alisema lengo ni kutoharibu uelewano wa wachezaji uwanjani ambao tayari kocha ameutengeneza, hivyo wanachotazama ni kuongeza nguvu kidogo katika idara ya ushambuliaji na safu ya ulinzi.

"Hatuwezi kubadili timu nzima kama Yanga, matarajio yetu ni kusajili mabeki wawili ama watatu na washambuliaji wawili tu ili kuongeza nguvu," Manara alisema.

"Tutasajili mshambuliaji mmoja wa kimataifa na mmoja wa ndani na kwa upande wa beki ikiwezekana mmoja wa kimataifa na mwingine wa ndani, hatutaki kuwa kama Yanga ambayo msimu ujao unaweza kushuhudia ikisajili wachezaji 15 wapya [aliwananga watani zao]."

Simba ambayo tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, hiyo ikiwa ni kwa mara ya tatu mfululizo, itaiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Namungo FC ikiwa na tiketi ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, amewapongeza wachezaji kwa kutoa dozi kwa Yanga juzi, huku akiwataka sasa kuelekeza akili zao kwenye mechi zilizosalia Ligi Kuu ili kumaliza msimu vizuri.

"Tulicheza vizuri na wachezaji walitimiza majukumu yao uwanjani na ndicho kimesababisha kupata ushindi mnono wa mabao 4-1 na kuleta furaha kwa Wanasimba wote," alisema.

Hata hivyo, raia huyo wa Ubelgiji alikiri kuwa Yanga ilikuwa bora zaidi katika dakika 15 za mwanzo ambapo walikuwa na kasi na kufanya mashambulizi ya haraka na baada ya kupata bao lao, lakini Simba ilikuwa bora katika muda wote uliobaki.

"Nimefurahishwa na jinsi ambavyo wachezaji wangu walivyocheza walijituma na walitimiza wajibu wao uwanjani kingine ni ushindi mnono tuliopata katika mchezo wa 'dabi' si jambo dogo hili, nawapongeza sana wachezaji wangu," alisema Sven ambaye kesho atakiongoza kikosi chake kuivaa Mbao FC katika mechi ya Ligi Kuu itakayopigwa Uwanja wa Taifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live