Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yapoza machungu

40809 Pic+simba Simba yapoza machungu

Mon, 11 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Simba imeanza kula vyema viporo vyake vya Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui Shinyanga.

Kocha Patrick Aussems aliingiza sura mpya katika kikosi chake akimpa nafasi beki wa kati Paul Bukaba kucheza na Pascal Wawa.

Pia Aussems aliwatumia Haruna Niyonzima, Zana Coulibaly, Muzamiru Yassin ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisugua benchi.

Simba ikiwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imejiweka katika nafasi nzuri ya kufanya vyema katika mchezo wa Jumanne dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Simba itacheza na Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni mechi ya marudiano baada ya awali kunyukwa mabao 5-0 mjini Cairo, Misri.

Ushindi huo angalau utakuwa umepoza machungu ya mashabiki wake ambao walikosa furaha muda mrefu, baada ya timu yao kuboronga katika mechi mbili dhidi ya Al Ahly na AS Vita ya DR Congo ambayo pia iliinyuka mabao 5-0.

Matokeo ya jana yametoa taswira nzuri kwa Simba katika mwelekeo wake wa ligi baada ya kula vyema kiporo chake cha kwanza katika mechi 10 ilizokuwa haijacheza wakati timu nyingine zimecheza mechi 24.

Simba imefikisha pointi 36 katika msimamo wa ligi nyuma ya watani wao wa jadi Yanga yenye pointi 55 na Azam 48.

Mabao ya Simba katika mchezo huo ambao Mwadui ilizinduka dakika 45 za kipindi cha pili, yalifungwa na Meddie Kagere, Mzamiru na John Bocco.

Kagere alifunga bao kwa mpira wa kichwa dakika ya 21, akipokea krosi safi kutoka kwa kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama.

Dakika 26 Mzamiru alifunga bao la pili akipokea pasi ya kifua iliyopigwa na Bocco ambaye dakika tatu baadaye alifunga la tatu kwa kichwa akipokea krosi ya Niyonzima.

Simba ilianza kipindi cha pili kwa kushambulia baada ya dakika 48 Bocco kushindwa kufunga.

Niyonzima alimuwekea pasi ya mwisho Bocco lakini alishindwa kufunga kwa mara nyingine.

Bocco aliendelea kukosa nafasi za kufunga baada ya dakika 85 kushindwa kuweka mpira wavuni akiwa katika eneo la hatari la Mwadui.

Mshambuliaji machachari wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda alianzia benchi katika mchezo huo na aliingia kipindi cha pili kujaza nafasi ya Chama lakini hakucheka na nyavu.



Chanzo: mwananchi.co.tz