Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yapigwa mkwara

Mkwara Pic Data Simba yapigwa mkwara

Tue, 27 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MASHABIKI wa Simba kwa sasa furaha yao ni kuona timu yao ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini chama lao limepigwa mkwara mapema kabla ya leo Jumanne kushuka tena uwanjani kuvaana na Dodoma Jiji katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.

Simba inaongoza msimamo ikiwa na pointi 58 mbele ya Yanga yenye 57, lakini sasa mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Dickson Ambundo amesema hawatokubali kupoteza pointi mbele ya vinara na watetezi hao katika mchezo wao utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Simba inahitaji pointi tatu nyingine ili kuongeza pengo la pointi dhidi ya watani wao Yanga kabla ya kuja kuvaana kwenye pambano la Kariakoo Derby litakalopigwa mwezi ujao ambalo litatoa muelekeo wa bingwa wa msimu huu wa VPL.

Ambundo aliliambia Mwanaspoti wanakuja Dar wakiwa na lengo la kuchukua pointi tatu au kugawana pointi na sio kuacha hata pointi moja kwa mnyama, licha ya kukiri pambano litakuwa kali.

“Tunakuja huko lakini lengo letu ni ushindi, tukikosa hilo hata sare na sio kupoteza mchezo huu muhimu kwetu,” alisema Ambundo mwenye mabao matatu na kuasisti mabao sita msimu huu.

Mshambuliaji huyo alisema wanatambua ugumu wa mchezo huo, lakini kwa jinsi walivyojiandaa wanaamini watapambana ili kupata pointi kulingana na maelekezo ya makocha wao wakiongozwa na Mbwana Makatta.

Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa Februari 4, Dodoma ilikubali kichapo cha mabao 2-1, bao la ushindi la Wekundu wa Msimbazi likiwekwa kimiani na Bernard Morrison dakika ya 66 baada ya awali, Meddie Kagere kuitanguliza Simba dakika ya 30 na Cleophas Mkandala kusawazisha dakika tano baadaye.

Licha ya Simba kuwa na moto mkali, lakini wanapaswa kuwa makini na Dodoma, ambayo juzi kati ilikaribia kuiumbua Azam baada ya matajiri hao wa Chamazi kuchomoa mabao na kutoka sare ya 2-2 mjini Dodoma. Dodoma inawategemea Ambundo sambamba na kinara wao wa mabao, Seif Karihe na Anwar Jabir ambao msimu huu wapo moto kinoma.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz