Dar es Salaam. Mshambuliaji Adam Salamba amefunga mabao mawili akiiongoza Simba kuichakaza Dakahada ya Somalia kwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza wa Kundi C uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Simba mabingwa mara sita wa Kombe la Kagame wamepata ushindi huo wa kishindo pamoja na kocha Masoud Djuma kuanzisha wachezaji wengi wapya katika safu yake ya ushambuliaji pamoja na mkongwe Pascal Wawa katika safu ya ulinzi.
Mbali ya Salamba wafungaji wengine wa Simba katika mchezo huo ulioshudiwa na mashabiki wachache ni Marcel Kaheza aliyefunga kwa penalti dakika ya 14 na Rashid Juma dakika ya 45.
Simba ilianza mchezoa kwa kasi zaidi wakiwa na uchu wa kufika langoni mwa wapinzani wao Dakadaha wakafanikiwa ndani ya dakika ya nane.
Simba walionekana kuonana zaidi uwanjani kutokana na pasi zao kuwafikia na kutawala zaidi mpira suala ambalo lilikuwa linawapa wakati mgumu wapinzani wao hasa safu ya ulinzi ambayo imekosa umakini na kutokana na mashambulizi ya mfululizo langoni mwao.
Simba walionekana wazuri zaidi kipindi cha kwanza kutokana na mpira kuchezwa upande mmoja na kuwaacha Dakadaha kusubili makosa machache za viungo wa Simba wakipoteza pasi ndio wacheze, lakini ukuta wa unaongozwa na Pascal Wawa tulikuwa ni mgumu kwao kuweza kupenya.
Dakika ya 14, Kaheza aliwanyanyua mashabiki wa Simba baada ya kuipatia Simba bao la kuongoza kwa mkwaju wa penati baada ya Abbas Amin Mohammed kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la 18.
Simba hawakuonyesha kuridhika na matokeo waliyoyapata baada ya kuendeleza mashambulizi dakika 23 waliongeza bao la pili kupitia kwa Salamba akipokea pasi safi kutoka kwa Ally Shomari na kupiga shuti lililojaa wavuni.
Dakika za mwisho kipindi cha kwanza Dakadaha waliendelea kukosa umakini zaidi na kuwaruhusu Simba kuendeleza kuzesha langoni mwao Mwinyi Kazimoto alimtengenezea nafasi Rashid Juma ambaye alikwamisha mpira nyavuni na kuifanya Simba inamaliza kipindi cha kwanza ikiwa mbele kwa mabao 3-0
Kipindi cha pili Simba imeendeleza ubora wao kwa Dakadaha kwa kuendeleza kuumiliki zaidi mpira kila idara na kuwafanya wapinzani wao washindwe kupiga shuti ata moja langoniĀ mwao.
Simba pamoja na kutawala mpira washambuliaji wao walikosa umakini kutokana na kushindwa kutumia nafasi walizotengeneza na kuishia kuchezea zaidi mpira eneo la katikati.
Dakika 76, Salamba aliandikia Simba bao la nne akiwa nje ya kumi na nane akipokea pasi safi kutoka kwa Kazimoto.
Ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa mabingwa hao wa kihistoria wa Kombe la Kagame ambao msimu huu wanapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa ubingwa huo.