Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yampa zawadi Mo

23469 Simba+pic TanzaniaWeb

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shangwe na furaha ya mashabiki wa Simba baada ya kupatikana mfadhaili mkuu Mohammed Dewji ‘Mo’ viliendelezwa na ushindi mnono wa mabao 3-0 ambao timu hiyo ilipata dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, jana.

Kwa takribani siku tisa alizokuwa ametekwa, mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla walikuwa katika simanzi na wengine walimuombea dua apatikane akiwa salama.

Dewji alitekwa alfajiri ya Alhamisi, Oktoba 11 na watu wasiojulikana alipokuwa akienda kufanya mazoezi ya viungo, kwenye ‘gym’ iliyopo ndani ya Hoteli ya Colosseum Oysterbay, jijini.

Mfanyabiashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 1.54 bilioni zaidi ya Sh3.5 trilioni kwa mujibu wa  Jarida la Forbes, alipatikana juzi  kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam baada ya kuachiwa na watekaji.

Jina la ‘Mo’ lilimbwa na kutajwa kwa nguvu kila Simba ilipofunga bao kuashiria kwa kiasi gani mfanyabiashara huyo maarufu alivyoteka hisia za mashabiki wa soka.

Katika kudhihirisha namna gani Simba ilipania kushinda mchezo huo, Kocha Patrick Aussems alijaza idadi kubwa ya wachezaji ambao kiasili wana tabia ya kushambulia badala ya kuzuia.

Kuanzia kwa kiungo namba sita hadi namba 11, Simba ilipanga wachezaji wenye tabia ya kushambulia ambao walikuwa sita na wanne walicheza nafasi ya ulinzi. Simba imefikisha pointi 17.

Mipango ya benchi la ufundi iliifanya timu hiyo kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Stand United ambayo yangeweza kuipatia ushindi mnono ingawa kikwazo alikuwa kipa Mohammed Makaka aliyeokoa mashuti mengi ya ana kwa ana.

Simba ilianza kuhesabu bao la kwanza dakika ya 31 baada ya kupata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo Cletus Chama aliyefunga kwa staili ya kuzungusha akiwa upande wa kulia mwa lango la Stand United.

Chama aliyepokea mpira kutoka kwa Shiza Kichuya alifanya juhudi binafsi za kumtoka beki wa Stand United kabla ya kupiga mpira uliomshinda Makaka.

Muda mfupi kabla ya mwamuzi kupuliza filimbi kuashiria muda wa mapumziko, Emmanuel Okwi aliifungia Simba bao la pili akimalizia pasi ndefu kutoka kwa Said Ndemla baada ya Simba kupoka mpira na kufanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa Stand United.

Kipindi cha pili Simba iliendeleza mashambulizi mfululizo langoni mwa Stand United na nusura kiungo Mohammed Ibrahim afunge bao la tatu, baada ya kuwatoka mabeki wawili lakini alijikuta akizuiwa na Makaka.

Dakika ya 66 Simba ilimtoa Ibrahim na kuingia Hassani Dilunga ambaye aliongeza kasi ya timu hiyo kwenye idara yake ya ushambuliaji.

Meddie Kagere aliipatia Simba bao la tatu dakika ya 77 akitumia vyema mawasiliano duni baina ya Makaka na mabeki wake katika harakati za kuokoa kona iliyopigwa na Mohammed Hussein 'Tshabalala'.

Bao hilo lilikuwa la sita kwa Kagere msimu huu baada ya kufunga dhidi ya Prisons, Mbeya City, Mwadui FC na African Lyon.

Simba ilifanya mabadiliko mengine kwa kuwatoa Kagere na Shiza Kichuya huku nafasi zao zikichukuliwa na Marcel Boniventure na Adam Salamba.

Kwa upande wa Stand ilimtoa pia Chinonso na nafasi yake kuchukuliwa na Jisendi Mathias.

Chanzo: mwananchi.co.tz