Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yamchanganya Zahera ubingwa wa Bara

34815 Pic+zahera Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amefunguka akiweka wazi ubingwa kuwa wanautaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini timu mbili Simba na Azam kama timu zinazomnyima usingizi kwenye mbio za kuwania ubingwa huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPL’.

Kikosi cha Mwinyi Zahera ambacho baadhi wako Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi, ndicho kinachoongoza kwenye msimamo wa Ligi hiyo, kikiwa na pointi 50, walizozikusanya kwenye michezo 18 kwa kushinda 16 na kutoka sare mara mbili.

Wapinzani wa Yanga kwenye mbio hizo za ubingwa ambao Zahera amewataja, Azam wapo kwenye nafasi ya pili, wakiwa na pointi 40 walizovuna kwenye michezo 17.

Simba SC ambao wapo nafasi ya tatu, wakiwa na pointi 33 wako nyuma michezo mitatu, ukilinganisha na Yanga ambao wanaongoza msimamo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Miamba hiyo ya soka ipo Zanzibar kucheza Kombe la Mapinduzi na leo itapambana na Chipukizi.

Zahera ambaye kikosi chake hakijapoteza mchezo hata mmoja kwenye Ligi, alisema kinachomnyima usingizi ni kasi walioyonayo wapinzani wake hao ambao wanamfukuza kwa ukaribu kwenye kilele cha msimamo wa TPL.

“Simba SC na Azam ndizo timu ambazo naona zinaweza kuleta upinzani kwetu kwenye kuwania ubingwa wa Ligi, sidhani kama zile timu ambazo zipo kuanzia nafasi ya nne zina nafasi ya kuchukua ubingwa kutokana na utofauti wa pointi uliopo.

“Mtibwa Sugar tumeicha pointi 24 ili watufikie ina amana tunatakiwa kupoteza michezo nane kitu ambacho sio rahisi kwetu kutokea, kibaya wakati sisi tunapoteza wao wanatakiwa washinde sio tupoteze wote.

“Lolote linaweza kutokea kwa sababu Simba SC wana michezo pungufu kama watashinda inaama presha itakuwa kubwa kwenye mbio za ubingwa,” alisema kocha huyo raia wa DR Congo.

Kocha huyo pia alisema mkakati wake ni kuhakikisha anapata pointi mbele ya timu hizo kwenye mzunguko huu wa pili ambao kuna baadhi ya klabu imeuanza ili kujitengenezea mazingira mapema ya kutwaa ubingwa huo.

Katika mzunguko wa kwanza Yanga ilivuna pointi moja mbele ya watani zao Simba, Septemba 30 mwaka jana mchezo baina yao na Azam wa mzunguko wa kwanza, unatarajiwa kuchezwa baada ya kumalizika kwa Kombe la Mapinduzi linaloendelea Zanzibar.

“Kama tutawafunga ina maana tutaendelea kuweka wigo mkubwa wa pointi baina yetu na wao, hicho ndicho kitu kinachotakiwa ili tujihakikishie ubingwa,” alisema Zahera

WANACHOSEMA WADAU

Baada ya Zahera kusema wapinzani wake wakuu kwenye mbio za ubingwa ni Simba na Azam , wadau mbalimbali wa soka wameibuka na kutoa mitazamo yao.

Naye kiungo wa zamani wa Yanga na Simba , Ally Yusuph ‘Tigana’ alitoa nafasi kubwa kwa Yanga na Azam kuchukua ubingwa wa Ligi kutokana na namna ambavyo Simba inavyoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo watatumia huko nguvu kubwa. Alisema maandalizi watakayofanya Ligi ya Mabingwa yatakuwa makubwa na watadharau ya Ligi Kuu na hapo ndipo watakapopotea, kwani Yanga na haina mambo mengi.

“Kama Simba wanataka kuchukua ubingwa basi wanatakiwa kufanya kazi ya ziada maana wanamichuano mingi ambayo ipo mbele yao, Azam na Yanga wao wapo hapa hapa na hesabu zao zote pamoja na kuwa kwenye michuano mingine ila kwa kiasi kibwa wamezielekeza kwenye Ligi,” alisema.

Beki wa zamani wa Simba SC, Boniface Pawasa alisema huu ndio muda wa kuanza kujitengenezea mazingira ya kutwaa ubingwa na hakupingana na kauli ya Zahera kwa kusema utofauti wa pointi unaanza kuziondoa Mtibwa na wengineo.

Wakati huo huo, Simba iliyopeleka kikosi kamili Kombe la Mapinduzi, inashuka uwanjani leo saa 2:15 usiku kucheza na Chipukizi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Simba itautumia mchezo huo kama sehemu ya mazoezi kujiandaa na mechi yake ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya JS Saoura wiki ijayo.

Mechi nyingine za juzi, Azam ilitoka sare ya 1-1 na Jamhuri wakati Mlandege iliilaza Chipukizi bao 1-0.



Chanzo: mwananchi.co.tz