Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yakwama kuishusha Yanga

28542 Simba+pic%255C TanzaniaWeb

Sun, 25 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabingwa wa soka nchini, Simba leo (Novemba 23) walitawala mchezo wao wa kiporo wa Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Lipuli FC ya Iringa, lakini wakalazimishwa sare ya bila kufungana katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini hapa.

Simba, ambayo imeizidi Yanga kwa idadi ya mechi, ilitakiwa iibuke na ushindi dhidi ya Wana Paluhengo ili irejee katika nafasi ya pili baada ya jana kushushwa na Yanga, ambayo iliitandika Mwadui kwa mabao 2-1 mkoani Shinyanga, lakini ikajikuta ikipeleka mashambulizi wakati wote bila ya kuzaa matunda

Hii ni mechi ya pili kwa Simba kulazimishwa sare msimu huu na hadi sasa imeshapoteza pointi saba, zikijumlishwa na matokeo ya kipigo mbele ya Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Azam inaongoza Ligi ikiwa na pointi 30 na kufuatiwa na Yanga yenye ponti 29, huku Simba ikiwa na pointi 27.

Lipuli, ambayo inaonekana kuwa mwiba mkali kila inapokutana na vigogo hao wa Mtaa wa Msimbazji, sasa imefikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi 14 na hivyo kupanda hadi nafasi ya 13, ikiwa imeizidi Stand United ya Shinyanga kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alifanya mabadiliko machache katika kikosi chake kilichoanza leo kutokana na kutokuwepo kwa Emmanuel Okwi, ambaye bado hajarejea tangu aende kuitumikia Uganda, na Shomari Kapombe ambaye ameumia.

Badala yake, Bocco alianza pamoja na Kagere katika safu ya ushambuliaji huku katika kiungo kukiwa na Jonas Mkude, Shizya Kichuya, ambaye baadaye alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga na Cletus Chama.

Nafasi ya Kapombe ilishikwa na Paul Mokaba, ambaye pia alitoka kumpisha James Kotei.

Kikosi hicho kiliweza kuichana ngome ya Lipuli lakini kikashindwa kuzigusa nyavu zilizolindwa na kipa Mohamed Yusuph.

Simba ilitawala sehemu ya kiungo na kupeleka mashambulizi mfullulizo golini mwa wageni, lakini washambuliaji wake walipoteza nafasi nyingi walizopata, ikiwemo ya dakika za mwisho wakati Erasto Nyoni alipopiga majalo golini mwa Lipuli na mpira kumkuta Rashid Juma aliyeunganisha, lakini mpira ukatambaa mbele ya goli na kutoka nje.

Lipuli pia itabidi impongeze kipa wake Yusuph, ambaye licha ya mashuti mengi kumlenga, alikuwa makini kuchungulia mipira iliyopenyezwa kwenye ukuta mnene wa ngome yake na kuidaka kirahisi.

Ikiongozwa na beki wa kati, Ally Mtoni 'Sonso, ambaye mwishoni mwa wiki alipangwa kwa mara ya kwanza kuanza katika kikosi cha Taifa Stars, Lipuli ilijibu mashambulizi ya Simba mara kadhaa na kukaribia kufunga wakati mshambuliaji wake, paul Nonga alipounganisha vibaya krosi huku kipa Aishi Manula akiwa ameshapotea.

Sonso alionekana kama amepewa kazi maalumu ya kumchunga Bocco na wakati wote alikuwa akifuatana naye.

Simba: Aishi Manula, Mohamed Hussein , Erasto Nyoni, Paul Bukaba (James Kotei dk 39), Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza Kichuya (Haruna Niyonzima, 75), Cloutus Chama, Meddie Kagere, John Bocco na  Hassan Dilunga (Rashid Juma, 46).

Lipuli FC: Mohamed Yussuph, William Lucian ‘Gallas’, Paul Ngelema, Ibrahim Job (Novaty Lufunga, 62), Ally Sonso, Freddy Tangalu, Steven Mganga, Mussa Nampaka (Shaaban Ada, 66), Paul Nonga, Zawadi Mauya na, Miraji Athumani.



Chanzo: mwananchi.co.tz