Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yajipigia Coastal

56433 SIMBA+PIC

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabao ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao jana walifunga mabao matatu kila mmoja, yameipa nafasi Simba kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kuichapa Coastal Union 8-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba imeshika usukani wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza ambapo mara ya mwisho ilikuwa Septemba mwaka jana na baada ya hapo ilitoa nafasi kwa Yanga na Azam kupokezana kijiti.

Kagere anaongoza chati ya wafungaji katika Ligi Kuu akifikisha mabao 20 akifuatwa na Heritier Makambo (Yanga), na Salim Aiyee wa Mwadui ya Shinyanga wenye magoli 16. Emmanuel Okwi amemfikia nyota mwenzake wa Simba, John Bocco katika magoli 14.

Simba ambayo jana ilicheza mechi yake ya 31, imeiporomosha Yanga yenye pointi 80 baada ya kufikisha pointi 81 katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20 za Tanzania Bara.

Yanga iliyocheza mechi 34 kesho inaweza kurejea kileleni endapo itaifunga Biashara United kwenye Uwanja wa Karume, mkoani Mara.

Coastal iliyoripotiwa kuwasili jana muda mfupi kabla ya mechi hiyo kwa basi ikitokea Tanga baada ya safari ya zaidi kilometa 332, imeweka rekodi ya kipigo kikubwa zaidi katika ligi msimu huu hadi sasa na imebaki katika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 41 baada ya mechi 34.

Katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja, Coastal ilionekana kucheza kichovu na haikuonyesha dhamira ya kutaka ushindi.

Wachezaji wa timu hiyo walizidiwa katika idara zote na hawakuonyesha ufundi au kutoa upinzani kwa Simba ambayo ilitawala mchezo huo.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao Simba ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Kagere ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, timu hiyo ilionyesha soka maridadi tofauti na mechi ya jana.

Simba walianza walianza kwa kushambulia dakika 5, za mwanzo huku winga Rashid Juma akionekana akikosa utulivu katika eneo la ushambuliaji.

Dakika 11, Rashid Juma aliwekewa pasi nzuri ndani ya boksi ambayo alipiga shuti kali lililopanguliwa kipa wa Coastal Union, Soud Abdallah na kumkuta Okwi aliyefunga bao la kwanza.

Dakika 19, Simba ilifanya shambulizi la haraka ambalo Okwi alimpasi pasi Kagere ambaye alimpa tena mgongeo ambao Okwi alifunga bao la pili.

Dakika 34, viungo wa kati wa Simba Jonas Mkude na Said Ndemla walimuacha Raizin Hafidh aliyesogea eneo la hatari kabla ya kutandika kiki kali iliyomshinda kipa Aishi Manula na mpira kujaa wavuni.

Dakika 44, Ndemla alimuwekea pasi Kagere akiwa ndani ya boksi na kupiga shuti kali ambalo lilikwenda kugonga mwamba wa juu na kumkuta Okwi ambaye alimalizia kwa kupiga shuti ambalo lilipanguliwa na kipa Abdallah kabla ya mabeki wa Coastal kuokoa mpira huo.

Dakika 46 Clatous Chama alipiga krosi ambayo mabeki wa Coastal walishindwa kuokoa na kumkuta Okwi aliyepiga kiki na kufunga bao la tatu.

Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 65 kwa kumtoa Rashid na kuingia Hassani Dilunga. Dakika ya 69 Kagere alifunga bao la nne kwa kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na Chama.

Mchezaji huyo raia wa Rwanda alifunga bao la tano dakika ya 75 kwa shuti la chini. Dakika 78 Simba ilimtoa Said Ndemla na kuingia Mohammed Ibrahim aliyetoa pasi kwa Dilunga aliyefunga bao la sita dakika ya 81.

Kagere alifunga bao la saba dakika ya 83 kabla ya Chama kuhitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la nane dakika za nyongeza.

Simba: Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohamed Hussein, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Clatous Chama, Said Ndemla, Meddy Kagere, Emmanuel Okwi na Rashid Juma.



Chanzo: mwananchi.co.tz