Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaitesa Mazembe

50430 SIMBSPIC

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

JAMANI hii Simba itabaki kuwa juu Afrika. Yaani zile taarifa kuwa ukikanyaga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hautoki salama zimesambaa hadi kuwafikia wababe wa soka la Afrika, TP Mazembe ambao wanateseka sana.

Si unajua pale Taifa wamechinjwa wababe wote kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo alianza JS Saoura ikala tatu bila safii kisha akaja Al Ahly akapigwa kidude kisha akajileta AS Vita naye akapigwa 2-1 na kuiacha Simba ikitinga hatua ya robo fainali. Sasa ni zamu ya TP Mazembe ambao, jana Jumatano ilitua jijini Dar es Salaam, lakini kwa hofu ilificha ratiba ya kuwasili kwao kwa ajili ya kuvaana na Simba.

Simba inaikaribisha TP Mazembe Jumamosi kwenye mchezo mgumu ikijipanga kwa ushindi, lakini wapinzani wao wanatetemeka unaambiwa.

Mazembe imechimba mkwara kuwa inataka kushinda mchezo huo ili kwenda kumaliza kazi Lubumbashi, DR Congo lakini Simba yenyewe inacheeka huku ikiwaita mashabiki wake kufika kwa wingi Taifa kwenda kuona wakiwazima Wakongomani hao.

Msafara wa Mazembe ulitua jijini Dar es Salaam, jana Jumatano ukitumia ndege yao binafsi ambayo huitumia wanapokwenda kucheza ugenini, ikiwa ni maalumu kwa wachezaji na benchi la ufundi.

Hata hivyo, mabosi wa Mazembe walitoa taarifa kuwa wangewasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, saa 7:00 mchana, lakini hadi kufikia muda wote haikuwa imejulikana walipo.

Nusanusa ya Mwanaspoti uwanjani hapo ambako kulikuwa na raia mbalimbali wa DR Congo waliokuwa wakisubiri kuwapokea, ikaelezwa wangetua saa 10:00 jioni ambako nako ikawa hadithi tu.

Mashabiki hao wa DR Congo wakiwa na bendera na skafu zenye rangi za Mazembe na DR Congo, ulikuwa umepigwa butwaa wakiwasubiri wababe hao bila mafanikio.

Hata hivyo, Mwanaspoti likabaini kuwa msafara wa kikosi hicho ungewasili majira ya jioni, ambapo katika kusaka ukweli ikabaini kuwa ndege ya Mazembe ilitua Uwanja wa Kimataifa wa Songwe jijini Mbeya. Ilipofika saa 12:30 jioni Mazembe wakakanyaga ardhi ya Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti uwanjani hapo, Patrick Kasangala ambaye ni mmoja wa waratibu wa Mazembe hapa nchini, alisema kikosi kiko salama na kilitua Mbeya kwa ajili ya kujaza mafuta.

Alisema waliamua kutua Mbeya kwanza kisha kuendelea na ratiba nyingine na suala la ratiba kubadilika hilo liko mikononi mwao. Pia, alisema ndege yao ilianza safari kutokea Afrika Kusini kwenda Lubumbashi kuwachukua wachezaji tu.

WAKWEPA BASI, HOTELI

Kama taratibu zilivyo ambako wageni hupokewa na kutayarishiwa huduma muhimu na wenyeji, kwa Mazembe ni mambo tofauti, unaambiwa. Simba imeandaa basi kwa ajili ya kuwabeba wachezaji na viongozi wa TP Mazembe, lakini wenyewe wametayarisha basi kwa ajili ya wachezaji na viongozi wao.

“Tunafahamu Simba wametuandalia gari, hayo watapanda viongozi na watu wengine na wachezaji watapanda hizi ambazo tumeandaa wenyewe,” alisema Patrick.

Kwa mujibu wa Patrick, kikosi cha Mazembe kitaweka kambi Hoteli ya Serena huku awali ikiaminika wangefikia kuwa Hyatt Kilimanjaro ila wakachomoa.

“Tumejitafutia hoteli wenyewe, hatujui kama Simba wametuandalia hoteli kwa ajili ya wachezaji na viongozi wetu,” aliongeza Patrick.

JKT YAWEKWA KIPORO

Jana Jumatano Simba ilikuwa isake ushindi wa 11 mfululizo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania, lakini mvua ikatibua mambo. Mvua zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini zimesababisha mchezo huo kuahirishwa baada ya Uwanja wa Jamhuri, kujaa maji na sasa utapangiwa tarehe. Mechi hiyo ambayo ilikuwa ya kiporo ilitakiwa ichezwe jana Jumatano, lakini haikuwa rahisi kuendelea kutokana na mvua hizo.

Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA), Charles Mwakambaya alisema uamuzi huo umetolewa baada ya uwanja kujaa maji kiasi cha mpira kushindwa kudunda.



Chanzo: mwananchi.co.tz