Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaingia mawindoni kwa Azam

78970 Simba+pic

Tue, 8 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

NYOTA wa Simba leo Jumatatu wanaendelea na mazoezi yao, jijini Dar es Salaam kabla ya kesho Jumanne kuanza safari kwenda Kigoma kuwafuata wababe wao waliowatoa nishai kwenye michuano ya Kombe la FA msimu uliopita, yaani Mashujaa FC kwa mchezo wa kirafiki.

Kama umesahau, ngoja tukukumbushe. Mashujaa ndio waliowatibulia Simba kwa kuwatupa mapema nje ya michuano ya FA msimu uliopita kwa kuwafumua mabao 3-2 katika mechi kali iliyopigwa kwwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Katika kuhakikisha wanajiweka sawa kabla ya kuvaana na Azam FC wiki mbili zijazo, Simba imepanga kucheza mechi mbili za kirafiki zitakazopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.

Mbali na Mashujaa waliopo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambako inaendelea kuwasha moto kwa kugawa dozi kwa wapinzani wake, pia Simba itavaana na Mabingwa wa Burundi, Aigle Noir mchezo utakaopigwa pia mjini humo. Noir ilitolewa kama Simba katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kupigwa mabao 5-1 dhidi ya Gor Mahia katika mechi ya marudiano mjini Nairobi. Mechi yao ya kwanza Burundi walitoka 0-0. Kwa mujibu wa Mratibu wa Simba, Abbas Ali Seleman, kikosi hicho kinachoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa alama zao 12 baada ya mechi nne, itaondoka kesho na mchezo wao wa kwanza utapigwa keshokutwa Jumatano dhidi ya Mashujaa.

“Kila kitu kipo sawa na huenda kikosi kikaondoka Jumanne kwa ajili ya michezo miwili ya kirafiki kujiandaa na mechi yetu ijayo ya Ligi Kuu dhidi ya Azam. Timu nyingine tutakayocheza nayo ni Aigle Noir de Makamba ya Burundi,” alisema.

Simba ambao wanalisaka taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu Bara, jana Jumapili iliwapa mapumziko mafupi wachezaji wake kabla ya leo kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, huku Kocha Patrick Aussems akiomba mechi hizo mbili.

Pia Soma

Advertisement
Aussems alisema, kwa vile ligi itasimama kupisha mechi za kimataifa, wasipopata mechi za kujipima nguvu inaweza kuathiri wachezaji wake, kwani kwa bahati mbaya ni kwamba wapinzani wao wameendelea kucheza mechi za Ligi Kuu.

Azam iliyokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho, ilikuwa ikila viporo vyake ambapo juzi ilivaana na Namungo na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kuchupa hadi nafasi pili nyuma ya Simba kwa kufikisha alama 9.

Msimu uliopita, Simba iliwatandika Azam mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza kabla ya kutoka suluhu waliporudiana mapema mwaka huu.

Timu hizo ndizo zilizofungua pazia la msimu huu kwa kupambana katika mechi ya Ngao ya Jamii ambapo Simba ilitakata kwa ushindi wa mabao 4-2, hali inayoashiria mechi yao ijayo itakayochezwa Oktoba 23 itakuwa yenye upinzani mkali zaidi.

Katika hatua nyingine, imeelezwa mabosi wa Simba wamemalizana na kiungo wao Jonas Mkude aliyekuwa na tuhuma za utovu wa nidhamu wa kukacha safari ya Kanda ya Ziwa ambapo walicheza na kushinda dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema ishu ya Mkude imemalizwa baada ya jamaa kukiri makosa yake na kuomba msamaha na kuelezwa atakatwa sehemu ya mshahara wake kama faini ya alichokifanya, huku akionywa asirudie tena utovu wa nidhamu.

Hakuna kiongozi yeyote aliyekuwa tayari kuelekeza suala hilo la Mkude kwa madai lilikuwa mikononi mwa Mtendaji Mkuu wa klabu, Senzo Mazingisa asiye na utamaduni wa kuulizwa au kujibu jambo lolote kupitia simu.

Hata hivyo, mmoja ya watu walio karibu na uongozi wa Simba alisisitiza msala wa Mkude umeisha na huenda akafuatana na timu safarini Kigoma kwenye mechi zao za kujipima nguvu kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kuwakabili Azam FC.

Chanzo: mwananchi.co.tz